CHINA-MAREKANI-USHIRIKIANO

Marekani yafutilia mbali madai ya Beijing katika Bahari Kusini mwa China

Mvutano kati ya Marekani na China unaendelea.
Mvutano kati ya Marekani na China unaendelea. Greg Baker / AFP

Marekani imetupilia mbali madai ya China ya kutaka kudhibiti rasilmali katika bahari inayozozaniwa ya Kusini, hatua ambayo inaweza kuzidisha mvutano kati ya nchi hizi mbili zilizostawi kiuchumi duniani.

Matangazo ya kibiashara

Marekani imepinga madai ya China kuhusu bahari iliyoko Kusini mwa China, na badala yake kukubaliana na Vietnam, Ufilipino pamoja na washirika wake wengine katika kanda hiyo.

Beijing haina ushahidi wowote wa kisheria ili kuonyesha kuwa ina haki ya kudhibiti rasilmali katika bahari ya Kusini mwa China na imetumia nguvu katika kipindi cha miaka kadhaa ya vitisho dhidi ya mataifa mengine ya kanda hiyo huko Asia Kusini, amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo.

"Tunataka kuwa wazi: madai ya Beijing kuhusu rasilimali za pwani katika Bahari ya China Kusini ni kinyume cha sheria kabisa, kwani ni kampeni ya vitisho ili kuweza kudhibiti eneo hilo," amesema katika taarifa.

"Ulimwengu hautaruhusu Beijing kutumia Bahari ya China Kusini kama sehemu yake ya baharini," ameongeza Mike Pompeo.

Kwenye taarifa, Pompeo pia aliyapinga madai ya China kuhusu umiliki wa kisiwa kinachozozaniwa cha Spratly, ambacho mapema mwaka huu, China ilitangaza kuwa ni wilaya inayoisimamia, hali ambayo itaiwezesha kutanua mipaka yake baharini.

Katika taarifa iliyotumwa kwenye tovuti yake, ubalozi wa China huko Washington imesema madai ya vitisho "hayana msingi wowote".

"Marekani sio nchi inayohusika moja kwa moja katika mambo hayo, lakini inaendelea kuingilia suala hilo," ubalozi wa China Washington umebaini.