URUSI-WHO-CORONA-AFYA

Coronavirus: Urusi yaripoti kesi mpya 6,248 za maambukizi

Urusi imekuwa nchi ya nne kuathirika zaidi duniani, baada ya Marekani, Bresil na Mexico.
Urusi imekuwa nchi ya nne kuathirika zaidi duniani, baada ya Marekani, Bresil na Mexico. REUTERS/Tatyana Makeyeva/File Photo

Urusi imerekodi visa vipya 6,248 vya maambukizi ya virusi vya Covid-19 leo Jumanne na kufanya jumla ya watu 739,947 walioambukizwa virusi hivyo nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Urusi imekuwa nchi ya nne kuathirika zaidi duniani, baada ya Marekani, Bresil na Mexico.

Maafisa wa afya wamerekodi vifo vipya 175 katika muda wa saa 24 zilizopita. Kufikia sasa Ugonjwa wa Covid-19 umeua watu 11,614 tangu ulipozuka nchini Urusi.

Hayo yanajiri wakati Shirika la Afya Duniani linaonya kuwa janga la Covid-19 linaendelea kuwa baya zaidi ulimwenguni na kwamba huenda hali ya kawaida iliyokuwepo zamani isirejee hivi karibuni.

Idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona imepindukia watu milioni 13 ulimwenguni, na zaidi ya watu 570,000 wamefariki, huku Marekani ikiendelea kurekodi idadi ya juu ya maambukizi mapya.

Mkuu wa shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amezitaka nchi kuweka mkakati kabambe wa kukabili idadi inayozidi kuongezeka ya maambukizi mapya, huku akisema kuwa nusu ya jumla ya maambukizi mapya hutokea mataifa ya Amerika.

Kwa upande wake Dkt Mike Ryan, Mkurugenzi wa dharura katika shirika la Afya Duniani, amesema kuwa kulegeza masharti ya kutotoka nje katika nchi za Amerika na kufungua baadhi ya maeneo kumesababisha maambukizi kuongezeka kwa kiasi kikubwa''.