HONG KONG-CORONA-AFYA

Coronavirus: Uvaaji wa barakoa ni lazima Hong Kong, mikusanyiko ya watu wawili yaruhusiwa

Mikusanyiko ya watu zaidi ya wawili imepigwa marufuku huko Hong Kong, kuanzia Julai 29, 2020, isipokuwa kwa familia tu.
Mikusanyiko ya watu zaidi ya wawili imepigwa marufuku huko Hong Kong, kuanzia Julai 29, 2020, isipokuwa kwa familia tu. Anthony WALLACE / AFP

Katika wiki za hivi karibuni, Hong Kong, koloni la zamani la Uingereza limeshuhudia ongezeko la visa vya maambukizi la Covid-19, na kusababisha mamlaka kuchukuwa hatua kali zaidi.

Matangazo ya kibiashara

Vifo vitatu na kesi mpya 145 vimeripotiwa Jumatatu, Julai 27, ikiwa ni rekodi mpya kwa Hong Kong, ambayo kwa siku sita mfululizo ilirekodi kesi mpya zaidi ya 100 kila siku.

Visa vingi vimepatikana katika nyumba za watumishi wanaostaafu.

Serikali imetangaza hatua mpya za kutokaribiana, ikiwa ni hatua kali zaidi tangu kuanza kwa mgogoro wa kiafya mwishoni mwa mwezi Januari katika eneo hilo.

Kiongozi namba mbili wa serikali ya Hong Kong, Matthew Cheung, amesema hali ya kiafya "inatiwa wasiwasi sana". Idadi ya watu kukusanyika imepunguzwa kutoka watu wanne hadi wawili, isipokuwa watu wa familia moja tu.

Kuhusu uvaaji wa barakoa, hatua ambayo wakazi wa eneo hilo la Hong Kong wamekuwa wakitekeleza kwa muda mrefu, sasa utakuwa ni lazima nje na katika maeneo ya umma. Watu wataruhusiwa kuvua barakoa wanapokunywa, kula au kutumia dawa, lakini sio kwa kuvuta sigara, kwa hatari ya kulipa faini ya euro karibu 200.

Ugonjwa wa Covid-19 umesababisha vifo vya watu 22 tu huko Hong Kong tangu kifo cha kwanza mwezi Februari, kwa wakazi karibu milioni 7.

Visa vya maambukizi ya hivi karibuni vimeonyesha kuwa maambukizi husambaa haraka katika familia na kupitia mawasiliano ya haraka na ya kila siku.