URUSI-USALAMA-SIASA

Kira Iarmych: Hali ya afya ya Alexeï Navalny haimruhusu kusafirishwa nje

Alexei Navalny, hapa ilikuwa Moscow, Februari 29, 2020.
Alexei Navalny, hapa ilikuwa Moscow, Februari 29, 2020. REUTERS/Shamil Zhumatov

Mpinzani mkuu nchini Urusi, Alexeï Navalny, ambaye yuko katika hali ya mahututi hosptalini baada ya madai ya kuwekewa sumu, hatasafirishwa nje ya nchi kwa sababu ya hali yake ya afya ambayo 'imedhoofika', msemaji wake amesema.

Matangazo ya kibiashara

Kira Iarmych pia ameshutumu uamuzi ambao 'anatishia maisha' ya mkosoaji huyo mkuu wa rais wa urusi Vladimir Putin".

"Daktari mkuu ametangaza kwamba Navalny hawezi kubebeka kwa minajili ya kusafirishwa nje ya nchi. Hali yake ya afya imezoroteka, "amesema Kira Iarmych kwenye ukurasa wake wa Twitter, akibaini kwamba 'ni hatari sana kumuacha katika hospitalini isiyo na huduma yoyote huko Omsk wakati hajafanyiwa vipimo vyovyote ".

Wakati huo huo msemaji wa ikulu Dmitry Peskov amesema kuwa wanamtakia afya njema-na kuwa mamlaka itaangalia suala la kuidhinisha matibabu nje ya nchi ikiwa itaombwa kufanya hivyo.

Inasemekana kuwa Ufaransa na Ujerumani zimependekeza kumpokea Alexeï Navalny ili aweze kupewa matibabu katika mazingira bora. Alilazwa Alhamisi asubuhi baada ya ndege iliokuwa ikimbeba kutoka Siberia kwenda Moscow kutua kwa dharura.

Alexei Navalny amepewa sumu kulingana na familia yake.

Alexei Navalny amekuwa mpinzani mkuu na mkosoaji mkuu wa Vladimir Putin tangu kuuawa kwa Boris Nemtsov mnamo mwaka 2015. Na hajawahi kukata tamaa: katika wiki za hivi karibuni aliunga mkono maandamano katika mkoa wa Khabarovsk. Pia alishutumu vikali marekebisho ya hivi karibuni ya Katiba yaliyopitishwa katika kura ya maoni, marekebisho ambayo yanamruhusu rais wa Urusi kuendelea kusalia madarakani hadi mwaka 2036.

Ushawishi wake wa kuhamasisha makumi ya maelfu ya watu kuingia mitaani ulisababisha aendelee kukaa gerezani.