KOREA KUSINI-CORONA-AFYA-ELIMU

Coronavirus: Shule zafungwa Seoul

Maafisa wa afya wanaonya kuwa kuna Korea Kusini hatari ya kukumbwa na mlipuko mbaya na kutoa wito kwa raia wake kuchukuwa hatua wenyewe ya kubaki ndani na kusitisha safari zisizokuwa na ulazima.
Maafisa wa afya wanaonya kuwa kuna Korea Kusini hatari ya kukumbwa na mlipuko mbaya na kutoa wito kwa raia wake kuchukuwa hatua wenyewe ya kubaki ndani na kusitisha safari zisizokuwa na ulazima. YONHAP / AFP

Korea Kusini imeagiza kufungwa kwa shule kadhaa katika mji mkuu Seoul na maeneo jirani na kurejelea visomo kupitia intaneti, hatua ya hivi karibuni iliyolenga kuzuia kuibuka tena kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Mamlaka ya afya yanchini Korea Kusini imeripoti kesi mpya 280 za maambukizi zilizothibitishwa katika muda wa saa ishirini na nne zilizopita, na kufanya jumla ya maambukizi kufikia 17,945 pamoja na vifo 310.

Hii ni ripoti ya kila siku ambayo imepungua ikilinganishwa na siku iliyotangulia ya kesi 397 ya kila siku, ambayo ilikuwa ya juu tangu mapema mwezi Machi.

Lakini wakati kesi nyingi mpya zimeripotiwa katika mji wa Seoul na maeneo jirani, maeneo yenye wakazi wengi, maafisa wa afya wanaonya kuwa kuna hatari Korea Kusini kukumbwa na mlipuko mbaya wa Corona na kutoa wito kwa raia wake kuchukuwa hatua wenyewe ya kubaki ndani na kusitisha safari zisizokuwa na ulazima.

Wizara ya elimu imesema kwamba wanafunzi wote - isipokuwa wanafunzi wa shule ya upili - katika miji ya Seoul na Incheon na mkoa wa Geonggi watafuata visomo kupitia intaneti hadi Septemba 11.

Kuanza kwa msimu wa pili wa masomo kuliahirishwa mara kadhaa tangu Machi, lakini shule nyingi nchini zilifunguliwa tena hatua kwa hatua kati ya Mei 20 na Juni 1 kutokana na kupungua kwa kesi mpya za kila siku za maambukizi.

Katika wiki mbili zilizopita, wanafunzi wasiopungua 150 na wafanyakazi 43 wa shule walipimwa na kupatikana na virusi vya Corona katika mji wa Seoul na maeneo jirani, Waziri wa Elimu Yoo Eun-hae amesema katika mkutano na waandishi wa habari.