HONG KONG-USALAMA-HAKI

Maandamano ya mwaka 2019 Hong Kong: Wabunge wawili wakamatwa

Kufikia sasa, polisi ya Hong Kong imeendelea kuwakamata wanaharakati wa demokrasia waliohusika katika maandamano ya mwaka 2019..
Kufikia sasa, polisi ya Hong Kong imeendelea kuwakamata wanaharakati wa demokrasia waliohusika katika maandamano ya mwaka 2019.. DALE DE LA REY / AFP

Wabunge wawili wa upinzani kutoka Hong Kong wamekamatwa na polisi kwa tuhuma zinazohusiana na maandamano dhidi ya serikali yaliyoukumba mkoa maalum wa utawala wa China mwaka jana, Chama kinachotetea democrasia Hong Kong kimesema.

Matangazo ya kibiashara

Polisi imethibitisha kwamba Lam Cheuk-ting na Ted Hui ni miongoni mwa watu takriban kumi waliokamatwa, lakini haikutoa maelezo zaidi.

Kulingana na ujumbe ulichapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Chama kinachotetea demokrasia, Lam amekamatwa kwa tuhuma za ghasia zilizotokea Julai 21, 2019, wakati maandamano ya wanaharakati wa demokrasia yalipolikumba koloni la zamani la Uingereza.

Siku hiyo, waandamanaji katikati mwa jiji la Hong Kong walirusha rangi nyeusi kwenye Ofisi ya serikali ya Hong Kong, ambayo inawakilisha serikali kuu ya Beijing.

Wakati huo huo, katika wilaya nyingine karibu na mpaka na China Bara, kundi la watu karibu 100 lilishambulia wanaharakati wa demokrasia. Lam alilazwa hospitalini kutokana na majeraha aliyoyapata usoni baada ya kurusha moja kwa moja picha za shambulizi hilo.

Kufikia sasa, polisi imewashikilia watu 44 wanaoshukiwa kuhusika katika shambulio hilo kubwa.

Haijafahamika kilichopelekea mamlaka kumshukia Lam kusababisha ghasia wakati huo.