UJERUMANI-URUSI-NAVALNY-SIASA-USHIRIKIANO

Ujerumani: Navalny alipewa sumu ya Novichok

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexey Navalny, Septemba 8, 2019 huko Moscow.
Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexey Navalny, Septemba 8, 2019 huko Moscow. REUTERS/Tatyana Makeyeva

Ujerumani imesema kuna ushahidi tosha kuwa mwanasiasa wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny alipewa sumu ya Novichok inayoathiri "mishipa ya fahamu'.

Matangazo ya kibiashara

Vipimo hivyo vilifanywa katika maabara maalum ya jeshi la Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas mapema jana alimuita balozi wa Urusi Berlin kujadili hali hiyo.

Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuwa mwanasiasa huyo alinusurika kuuawa na ameongeza kuwa anatarajia Urusi kueleza msimamo wake.

“Hatima ya Alexei Navalny imevutia hisia za ulimwengu wote. Dunia itatafuta majibu kutoka kwa Urusi. Tutawafahamisha washirika wetu wa Umoja aw Ulaya na Jumuiya ay Kujihami ya Nchi za Magharibi, NATO, kuhusu matokeo haya ya uchunguzi. Tutashauriana na kuamua hatua mwafaka ya pamoja tutakayochukua kwa kutegemea na kuhusika kwa Urusi. Uhalifu dhidi ya Alexei Navalny ni kinyume na maadili na haki za msingi tunazozilinda” amesema Angela Merkel.

Viongozi kutoka kote ulimwenguni wamelaani tukio la kupewa sumu kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny katika jaribio la kutaka kumuuwa.

Sumu inayoathiri mishipa ya fahamu ya Novichok ilitumiwa kwa aliyekuwa jasusi wa Urusi Sergei Skripal na binti yake wakiwa Uingereza mwaka 2018. Ingawa wao walinusurika, mwanamke mwingireza alifariki baadae akiwa hospitalini. Uingereza ilishutumu jeshi la Uingereza kwa kutekeleza shambulio hilo.