BELARUS-UNSC-USALAMA-SIASA

Belarus: Kiongozi wa upinzani Tsikhanouskaya aomba msaada kwa Umoja wa Mataifa

Kiongozi wa upinzani nchini Belarus Svetlana Tsikhanouskaya.
Kiongozi wa upinzani nchini Belarus Svetlana Tsikhanouskaya. REUTERS

Kiongozi wa upinzani nchini Belarus Svetlana Tsikhanouskaya ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kulaani ukandamizaji uliopangwa na rais Alexander Lukashenko dhidi ya waandamanaji ambao wanalaani mazingira ambamo alichaguliwa kwa muhula mwingine katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Matangazo ya kibiashara

Akiongea katika mkutano kwa njia ya video mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mgombea huyo wa zamani wa upinzani pia ameomba Umoja wa Mataifa kutuma ujumbe wa uchunguzi kwa jamhuri hiyo ya zamani ya Sovieti.

Anataka pia Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa iandae kikao maalum kuhusu hali ya nchi inayoendelea katika nchi yake.

"Sisi wananchi wa Belarus tunahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa ili kukomesha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu dhidi ya binadamu unaoendelea," amesema.

Hii ni mara ya kwanza kwa Svetlana Tsikhanouskaïa, aliyekimbilia uhamishoni nchini Lithuania katika siku za kwanza kabisa za maandamano, kueleza kuhusu mgogoro wa kisiasa ambao haujawahi kutokea tangu Lukashenko aingie madarakani, mwaka 1994.

"Tunaomba Umoja wa Mataifa kulaani vikosi vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji," ameongeza wakati wa mkutano huo wa Baraza la Usalama.

Wajumbe wawili wa kudumu wa Baraza hilo, Urusi na China, ambao wana kura turufu, wameelezea upinzani wao kwa uingiliaji wowote wa nchi za kigeni katika maswala ya ndani ya Belarus.

"Jaribio la kutangaza hali nchini Belarus linaweza tu kufanya mambo kuwa mabaya zaidi," amesema Dmitri Poliansky, naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa.