INDIA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Idadi ya maambukizi yakaribia Milioni 5 India

India ni nchi ya tatu iliyoathirika zaidi na ugonjwa huo kwa idadi ya maambukizi baada ya Marekani na Brazil.
India ni nchi ya tatu iliyoathirika zaidi na ugonjwa huo kwa idadi ya maambukizi baada ya Marekani na Brazil. REUTERS

India imerekodi visa vipya 83,809 vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya Corona katika muda wa saa ishirini na nne zilizopita, ikiwa ni idadi ndogo ya kila siku kwa wiki, kulingana na takwimu zlizotolewa na Wizara ya Afya ya India.

Matangazo ya kibiashara

Kufikia sasa India ina wagonjwa milioni 4.93 na zaidi ya vifo 80,000, ikiwa ni pamoja na vifo 1,054 vilivyorekodiwa katika muda wa saa ishirini na nne zilizopita.

Wakati huo huo shirika la Afya Duniani, WHO, linasema vifo vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya Corona, vinatarajiwa kuongeka kati ya mwezi Oktoba na Novemba.

Mwakilishi wa WHO barani Ulaya Hans Kluge ametoa onyo hilo, licha ya kusema kuwa hivi karibuni, bara hilo limeshuhudia ongezeko la maambukizi lakini idadi ya vifo haijaongezeka sana.

Aidha, Kluge ameonya kuwa hata iwapo chanjo itapatikana, haitakuwa mwisho wa maambukizi hayo.

Bara la Ulaya lina maambukizi zaidi ya Milioni Mbili na vifo zaidi ya Laki Mbili.

Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa Covid-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.

Kufikia sasa kinachojulikana ni kuwa Covid-19, ni ugonjwa ambao unaothiri mfumo wa kupumua wa binadamu.

Dalili zake ni pamoja na homa kali, kukohoa ambako baada ya wiki moja muathiriwa anakabiliwa na tatizo la kupumua.