INDIA-MAJANGA ASILI

Ishirini waangamia baada ya jengo moja kuporomoka India

Maporomoko ya majengo yanaripotiwa mara kwa mara nchini India kati ya mwezi Juni na Septemba, wakati wa msimu wa masika, na mvua kubwa wakati mwingine inasababisha hasara kubwa.
Maporomoko ya majengo yanaripotiwa mara kwa mara nchini India kati ya mwezi Juni na Septemba, wakati wa msimu wa masika, na mvua kubwa wakati mwingine inasababisha hasara kubwa. AFP

Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na kuporomoka kwa jengo la makazi la ghorofa tatu magharibi mwa India Jumatatu wiki hii imeongezeka hadi 20 na miili zaidi inatarajiwa kupatikana chini ya vifusi vya jengo hilo, maafisa wamesema leo Jumanne.

Matangazo ya kibiashara

Shughuli za uokoaji zinaendelea ili kupata manusura katika magofu ya jengo hilo lililoporomoka huko Bhiwandi, karibu na mji wa Bombay.

Siku ya Jumatatu, waokoaji kutoka Kikosi cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga (NDRF) waliweza kuokoa watu 20 wakiwa hai ikiwa ni pamoja na wavulana wawili wenye umri wa miaka minne na saba.

Msemaji wa Kikosi cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga (NDRF) amewaambia waandishi wa habari kuwa timu za uokoaji, zikisaidiwa na mbwa, walipata miili ishirini katika mabaki ya saruji na vifusi vya matofali ya jengo hilo lililoanguka Jumatatu kabla ya alfajiri.

Mkurugenzi mkuu wa NDRF, Satya Narayan Pradhan, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba wanatarajia kupata miili zaidi kutoka chini ya vifuzi vya jego hilo.

Sababu za tukio hilo hazijajulikana kwa sasa. Maporomoko ya majengo yanaripotiwa mara kwa mara nchini India kati ya mwezi Juni na Septemba, wakati wa msimu wa masika, na mvua kubwa wakati mwingine inasababisha hasara kubwa.