ARMENIA-AZERBAIJAN-USALAMA

EU yatoa wito wa utulivu Nagorno-Karabakh

Mapigano kati ya Armenia na Azerbaijan katika eneo la Nagorno-Karabakh, Septemba 28, 2020.
Mapigano kati ya Armenia na Azerbaijan katika eneo la Nagorno-Karabakh, Septemba 28, 2020. Defence Ministry of Azerbaijan/Handout via REUTERS

Mapigano makali kati ya wanajeshi wa Azerbaijan na Armenia yameendelea kuwania jimbo lenye utata la Nagorno-Karabakh katika mpaka wa nchi hizo mbili huku vifo vya raia vikiripotiwa.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano makali yalizuka kati ya wanajeshi wa nchi zote mbili Jumapili iliyopita kuhusu umiliki wa jimbo tata la Nagorno-Karabakh na kufikia siku ya Jumatatu, yamekuwa yakiendelea bila ya kuwepo kwa matumaini kuwa yatafika mwishoni hivi karibuni.

Haya ndio mapigano mabaya zaidi kuhusu kuwania jimbo hilo tangu mwaka 2016 na ripoti zinasema kuwa vifo vya raia na wanajeshi kutoka pande zote, vimeripotiwa.

Armenia imesema kuwa imewapoteza wanajeshi wake 31, na kupoteza baadhi ya ngome zake lakini imefanikiwa kuzidhibiti tena.

Azerbaijan inasema imesababisha maumivu makubwa dhidi ya wanajeshi wa Armenia, huku raia wake 26 wakijeruhiwa.

Mataifa mbalimbali duniani, yakiongozwa na Marekani, Urusi, Iran na Mataifa ya Ulaya, yametaka pande zote mbili kuacha makabiliano na kuanza mazungumzo.

Tangu mwaka 1991, nchi hizo mbili zimekuwa zikipambania jimbo la Nagorno-Karabakh lililojitangazia uhuru wake kutoka ka Umoja wa Kisoviet.