ARMENIA-AZERBAIJAN-USALAMA

Armenia: Tuko tayari kujadili na OSCE kusitisha mapigano Nagorno-Karabakh

Mapigano kati ya Armenia na Azerbaijan katika eneo la Nagorno-Karabakh, Septemba 28, 2020.
Mapigano kati ya Armenia na Azerbaijan katika eneo la Nagorno-Karabakh, Septemba 28, 2020. RFI/Elena Gabrielian

Armenia imesema iko tayari kujadili na Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) ili kusitisha mapigano katika eneo la Nagorno-Karabakh, Wizara ya Mambo ya nje ya Armenia imetangaza leo Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Mzozo kati ya vikosi vya Azerbaijan na vile vya Armenia, ambao ulisimama kwa miaka kadhaa huko Nagorno-Karabakh uliibuka tena Jumapili iliyopita.

Ufaransa, Marekani na Urusi, ambazo zinaongoza kundi la Minsk lililoundwa baada ya mzozo wa 1991, siku ya Alhamisi zilitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuwataka viongozi wa Armenia na Azerbaijani "kuanza tena mazungumzo, kwa nia njema na bila masharti yoyote, chini ya mwavuli wa viongozi wa OSCE".

Uturuki, ambayo inaunga mkono Azerbaijani, imefutilia mbali mpango huu.

Wakati huo huo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameshutumu uingiliaji wa makundi ya kjihadi katika mzozo wa Nagorno-Karabakh.

Emmanuel Macron anatarajia kumpigia simu rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kutaka "maelezo" kutoka kwake, rais Macron ametangaza leo Ijumaa, akitoa wito kwa Jumuiya ya kujihami ya nchi za Magharibi, NATO, "kuwa makini" kwa vitendo vya Ankara, mwanachama wa muungano huo.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari katika mkutano wa Umoja wa Ulaya Alhamisi hii huko Brussels, rais wa Ufaransa alizungumzia kinaga ubaga kuhusu mgogoro unaoendelea huko Nagorno-Karabakh.

"Kulingana na taarifa zetu za kijasusi, wapiganaji 300 waliondoka nchini Syria kwenda Baku wakipitia Gaziantep [nchini Uturuki]," Emmanuel Macron amesema. Wanajulikana, walifuatiliwa, na kutambuliwa, ni wanamgambo wa makundi ya jihadi wanaoendesha harakati zao katika mkoa wa Aleppo. Kikosi kingine kinajiandaa kwenda Nagorno-Karabakh. Mstari mwekundu umevukwa, haikubaliki."

Ufaransa, pamoja na Urusi na Marekani, ni sehemu ya OSCE "kundi la Minsk" linalohusika na kusuluhisha mzozo huu. "Nitampigia simu rais Erdogan katika siku chache zijazo kwa sababu kama mwenyekiti mwenza wa kundi la Minsk, ninafikiria kuwa ni jukumu la Ufaransa kuomba maelezo," ameongeza rais wa Ufaransa .

Mapigano yaliongezeka Alhamisi katika mkoa wa Nagorno-Karabakh licha ya wito mpya wa kusitisha mapigano. Eneo hili, ambalo lina watu wengi, raia wa Armenia, lilikuwa limejitenga na Azerbaijan, na kusababisha vita mwanzoni mwa miaka ya 1990, ambayo ilisababisha vifo vya watu 30,000.