ARMENIA-AZERBAIJAN-USALAMA

Nagorno-Karabakh: "Suluhisho pekee ni kuondolewa kwa jeshi la Armenia"

Rahman Mustafayev, Balozi wa Azerbaijan nchini Ufaransa.
Rahman Mustafayev, Balozi wa Azerbaijan nchini Ufaransa. RFI / Véronique Gaymard

Wakati mapigano yakiendelea huko Nagorno-Karabakh, Balozi wa Azerbaijan nchini Ufaransa, H.Rahman Mustafayev, amesema kwamba suluhisho pekee la kusitisha mapigano ni kuondolewa tu kwa wanajeshi wa Armenia katika eneo hilo lililojitenga.

Matangazo ya kibiashara

Katika mahojiano na RFI, balozi H.Rahman Mustafayev amesema "hii ni vita ya kweli. Tangu Julai, jeshi la Armenia limekuwa likifanya uchochezi unaoendelea kwenye maeneo ya mipaka rasmi na pia kwenye masuala ya mawasiliano katika mkoa wa Nagorno-Karabakh wa Azerbaijan".

Tangu mwezi Julai, jamii ya kimataifa haijazungumza chochote. Kwa hivyo labda Armenia ilijisikia huru kuona kuwa yote yanawezekana, amebaini balozi wa Azerbaijan nchini Ufaransa.

Mapigano yanaendelea huko Nagorno-Karabakh kwa kasi kubwa. Wengi wanahofu kuwa mzozo huo utagubika eneo lote. Alhamisi, Oktoba 1, viongozi wa nchi za kundi la Minsk (Urusi, Ufaransa, Marekani) walizitaka pande hizo mbili, Armenia na Azerbaijan, kusitisha mapigano mara moja.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres jana Ijumaa alitoa tena wito kwa nchi hizo mbili "kumaliza uhasama wao mara moja."