Armenia na Azerbaijan zashtumiana, Ufaransa, Marekani na Urusi zataka mapigano kukoma
Imechapishwa:
Wakati huu mataifa ya Armenia na Azerbaijan yakiendelea kuzozania jimbo la Nagorno-Karabakh kwa wiki mbili sasa, pande zote mbili zinaendelea kulaumiana kuhusu mashambulizi ambayo yanazidi kuhatarisha maisha ya raia wa kawaida.
Mapingano hayo yameingia siku ya 10 wiki hii, huku pande mbili zinazozana zikipuuzia mbali wito wa kimataifa wa kusitisha vita, Azerbaijan ikitaka Uturuki kuhusishwa katika utafutaji wa suluhu.
Wakati huo huo Ufaransa, Marekani na Urusi zimezitaka Armenia na Azerbaijan kukubaliana kusitisha mapigano bila masharti baada ya nchi hizo jirani kuanza kurushiana makombora kwenye miji mikubwa na kuuongeza mzozo wao wa kuligombania eneo la Nagorno-Karabakh.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu wamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba mzozo unaozidi kuongezeka ikiwemo mashambulizi yanayodaiwa kuvilenga vituo vya kiraia ni kitisho kisichokubalika kwa utulivu wa ukanda huo.
Mapigano hayo yamesababisha takriban watu 260 kuuawa, na wengine kulazimika kuyatoroka makazi yao na kukimbilia maeneo salama.