ARMENIA-AZERBAIJAN-URUSI-USALAMA

Nagorno-Karabakh: Azerbaijan na Armenia zakubaliana kusitisha mapigano

Mawaziri wa mambo ya nje wa Azabajani, Urusi na Armenia wakati wa mazungumzo Oktoba 9, 2020 huko Moscow.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Azabajani, Urusi na Armenia wakati wa mazungumzo Oktoba 9, 2020 huko Moscow. AFP Photos/RUSSIAN FOREIGN MINISTRY/Handout

Azerbaijan na Armenia zimeafikiana kusitisha mapigano kuanzia saa sita Jumamosi katika jimbo lililojitenga la Nagorno-Karabakh, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imetangaza baada ya mazungumzo kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Armenia na Azerbaijan huko Moscow.

Matangazo ya kibiashara

Jitihada za kidiplomasia za siku zilizopita zimezaa matunda. makubaliano ya kusitishwa mapigano yamefikiwa kati ya pande mbili hasimu "kwa sababu za kibinadamu".

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano yatawezesha nchi hizo mbili "zoezi la kubadilishana wafungwa wa kivita, watu wengine na miili ya waliouawa kulingana na vigezo vya Kamati ya Msalaba Mwekundu".

Mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mzozo yatafanyika kati ya Azerbaijan na Armenia. "Azerbaijan na Armenia pamoja na kundi la upatanishi wa wenyeviti wenza wa OSCE Minsk Group [...] wamekubaliana kufanya mazungumzo ili kufikia haraka suluhu ya amani" ya mzozo huko Nagorno-Karabakh , imesema taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya nje ya Urusi, iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo.

Wiki mbili za mapigano

"Vigezo maalum" vya utekelezaji wa usitishaji vita vitaafikiwa baadaye, ameongeza Sergey Lavrov. Mazungumzo haya kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Armenia na Azerbaijan huko Moscow yamedumu zaidi ya saa 10 na yamemalizika usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi.