Nagorno-Karabakh: Mapigano yarindima katika mji wa Hadrut
Mkataba wa kusitisha mapigano kati ya wanajeshi wa Armenia na Azerbaijan kuhusu mmilili wa jimbo la Nagorno-Karabakh umevunjika baada ya wanajeshi kutoka pande zote mbili kurejelea mapigano siku ya Jumatatu.
Imechapishwa:
Mapigano yameanza tena, licha ya wasuluhishi wa mzozo huu kutoka Jumuiya ya Kimataifa kuanza mchakato wa kupata suluhu ya kudumu kuhusu mzozo huu kwa kuanza mazungumzo.
Armenia na Azerbaijan kwa kipindi cha wiki mbili zimeendeleza mapigano katika jimbo la Nagorno-Karabakh, linalokaliwa na jamii ya watu wa Armenia lakini linadhibitiwa na Azerbaijan, huku kila upande ukitaka kudhibiti.
Watu zaidi ya Mia tatu kutoka pande zote mbili wamepoteza maisha na makaazi kuharibiwa tangu kuzuka kwa vita hivi ambavyo vinaelezwa kuwa vibaya tangu mwaka 1994 wakati nchi hizo mbili zilipotia saini mkataba wa maelewano kuhusu jimbo hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya mazungumzo ya zaidi ya saa 10 mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi hizo mbili, wakiwa jijini Moscow nchini Urusi, walikubaliana kusitisha vita kwa sababu za kibinadmu lakini pia kupitisha mazungumzo ya amani.
Armenia na Azerbaijan kila upande unalaumu mwenzake kwa kushindwa kuheshimu maelewano ya kusitisha vita, wakati huu kukiwa na hofu kuwa iwapo hali itaendelea hivyo, maafa yataongezeka.