KOREA KASKAZINI

Kim Jong Un aitaja Marekani kuwa ni 'adui mkubwa wa Korea Kaskazini'

Kim Jong Un, kiongozi wa Korea Kaskazini
Kim Jong Un, kiongozi wa Korea Kaskazini REUTERS/Stringer

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anasema Marekani ni "adui mkubwa" wa nchi yake, ikiwa ni taarifa ya uchochezi iliyoelekezwa kwa taifa hilo kubwa lenye nguvu duniani saa chache kabla ya rais mteule Joe Biden kuanza muhula wake.

Matangazo ya kibiashara

Kim Jong Un pia amehakikisha kuwa nchi yake inataka kupata manowari ya nyuklia, shirika la serikali la KCNA limeripoti leo Jumamosi, kwa mujibu wa Seoul.

Pyongyang "inapaswa kujikakamua na kujiendeleza ili kuikabili Marekani, kikwazo kikubwa kwa mapinduzi yetu na adui yetu mkubwa," Kim Jong Un amesema katika mkutano wa 8 wa chama tawala kulingana na shirika hilo.

Kauli yake inakuja chini ya wiki mbili kabla ya Joe Biden kuchukua wadhifa wa rais wa Marekani na wakati uhusiano kati ya Kim na rais anayemaliza muda wake Donald Trump umekuwa wenye mvutano mkubwa.

Baada ya kurushiana vijembe, matusi na vitisho vya vita vya nyuklia, Kim Jong Un na rais wa Marekani Donald Trump walijaribu kupatia ufumbuzi matatizo yao, baada ya mikutano kadhaa ya kihistoria.

Lakini hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana juu ya suala tata la mpango wa nyuklia na utengenezaji wa makombora ya masafa marefu kutoka Pyongyang.

Mazungumzo hayo yamekwama tangu kushindwa kwa mkutano wa pili kati ya wawili hao mwishoni mwa mwezi Februari 2019 huko Hanoi.

Moja ya sababu za mkwamo huu ni ukosefu wa maelewano juu ya ahadi ya Korea Kaskazini ili kuweza kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi yake.