BURMA-SIASA-HAKI

Burma: Aung San Suu Kyi ashtakiwa kwa makosa 2 mapya

Waandamanaji wanaopinga mapinduzi huko Yangon wakishikilia bango lililochorwa picha ya kiongozi wa zamani wa Burma Aung San Suu Kyi, Februari 17, 2021.
Waandamanaji wanaopinga mapinduzi huko Yangon wakishikilia bango lililochorwa picha ya kiongozi wa zamani wa Burma Aung San Suu Kyi, Februari 17, 2021. AFP - SAI AUNG MAIN

Kiongozi wa zamani wa Burma Aung San Suu Kyi, aliyetimuliwa katika mapinduzi ya kijeshi ya Februari 1, ameshtakiwa leo Jumatatu Machi 1 kwa makosa mawili mapya, kulingana na vyanzo kutoka kwa timu yake ya mawakili.

Matangazo ya kibiashara

Sasa anashtakiwa kwa kukiuka sheria ya mawasiliano ya simu na "kuchochea machafuko", wakili Nay Tu amesema.

Aung San Suu Kyi, anayezuiliwa katika sehemu isiyojulikana mpaka sasa tangu kukamatwa kwake, alikuwa tayari ameshtakiwa kwa kuingiza mazungumzo kwa njia isiyo halali na kwa kukosa kufuata vizuizi vinavyohusiana na virusi vya Corona.

Kumi nane wauawa katika maandamno

Hayo yanajiri wakati polisi nchini Burma iliwafyatulia risasi waandamaji jana Jumapili ikiwa ni siku mbaya kabisa ya umwagaji damu tangu maandamano yalipoanza wiki kadhaa zilizopita dhidi ya mapinduzi ya kijeshi.

Jana Jumapili Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ililaani ukandamizaji unaofanywa dhidi ya waandamanaji ikisema watu 18 waliuawa. Wtau watano waliuawa katika mji wa Yangon chanzo kutoka Umoja wa Mataifa kimebaini.

Wakati huo Gazeti la Myanmar Now liliripoti kuwa watu wawili waliuawa katika mji wa pili wa Mandalay.

Nchi mbalimbali zinaendelea kulaani ukandamizaji huo na ukatili vinavyoendeshwa na vikosi vya usalama nchini Burma.