BURMA

Jeshi la Burma ladai kuhuzunishwa na vifo vya waandamanaji

Kulingana na hesabu ya shirika linalotoa huduma kwa Wafungwa wa Kisiasa (AAPP), watu wasiopungua 261 wamepoteza maisha tangu kukandamizwa kwa maandamano na vikosi vya usalama vya Burma.
Kulingana na hesabu ya shirika linalotoa huduma kwa Wafungwa wa Kisiasa (AAPP), watu wasiopungua 261 wamepoteza maisha tangu kukandamizwa kwa maandamano na vikosi vya usalama vya Burma. REUTERS - STRINGER

Jeshi la Burma limetoa rambirambi zake kwa familia ya wahanga baada ya vifo vya waandamanaji 164 waliokuwa wakipinga mapinduzi ya kijeshi ya Februari 1, lakini limewashutumu watu hao kuwa ndio chanzo cha machafuko yanayoikumba nchi hiyo na vitendo vya uharibifu wa mali.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Burma, Naypyitaw, msemaji wa mamlaka ya kijeshi inayotawala, Zaw Min Tun, amesema amehuzunishwa "na vifo hivyo kwa sababu waliofariki dunia ni raia  wa Burma". Hata hivyo, amebaini kwamba maafisa tisa wa vikosi vya usalama pia waliuawa.

"Je! Tunaweza kusema kuwa waandamanaji hawa wanataka amani?" amehoji, huku akionesha video ya viwanda vilivyochomwa moto. "Ni nchi gani au shirika gani linaloweza kubaini kuwa vurugu hizi ni za amani?" Amehoji pia.

Zaw Min Tun pia ameshutumu vyombo vya habari kwa kueneza "habari za uongo" na kuchochea machafuko, hata kutishia waandishi wengine kwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Burma imetumbukia katika machafuko tangu jeshi lilipomkamata Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama cha NLD, ambaye chama chake kilishinda uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka jana.

Kulingana na hesabu ya shirika linalotoa huduma kwa Wafungwa wa Kisiasa (AAPP), watu wasiopungua 261 wamepoteza maisha tangu kukandamizwa kwa maandamano na vikosi vya usalama vya Burma.