Wakuu wa majeshi duniani walaani jeshi la Myanmar kwa kuwaua waandamanaji

Wanajeshi wa Myanmar
Wanajeshi wa Myanmar AFP/File

Wakuu wa Majeshi kutoka mataifa 12 duniani, yamelaani hatua ya jeshi la Myanmar kuendelea kuwashambulia waandamanaji, siku moja baada ya watu 114 kuuawa wakiwemo watoto.

Matangazo ya kibiashara

Mauaji ya Jumamosi ndio mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo la bara Asia, tangu kuanza kwa maaandamano ya wananchi tarehe 1 mwezi Februari, kutaka kuachiliwa huru kwa kiongozi wa kiraia Aung Suu Kyi.

Miongoni mwa wakuu wa majeshi waliolaani hatua hiyo ya jeshi la Myanmar, ni pamoja na wale kutoka Marekani, Uingereza, Japan na Korea Kusini

Wakuu hao wa Majeshi wamelitaka jeshi la kuacha kutumia nguvu dhidi ya wananchi na badala yake kufanya kazi ya kurejesha heshima ya wananchi wa Myanmar wanaodai haki yao.

Mchunguzi wa Umoja wa Mataifa, ameeleza kuwa mauaji ya Jumamosi yamehusisha watu wengi walioshiriki kwenye maandamano hayo.

Licha ya mauaji hayo, maandamano zaidi yameendelea kushuhudiwa katika miji miwili mikubwa nchini humoi Yangon na Mandalay huku mazishi ya watu waliouawa katika maandamano ya Jumamosi wakizikwa.