MYANMAR

Myanmar: Waandamanaji kumi na moja wauawa katika makabiliano mapya

Waandamanaji wanachoma nakala za Katiba ya Myanmar ya mwaka 2008 wakati wa maandamano dhidi ya mapinduzi ya kijeshi, katika mji wa Launglon, Myanmar Aprili 8, 2021.
Waandamanaji wanachoma nakala za Katiba ya Myanmar ya mwaka 2008 wakati wa maandamano dhidi ya mapinduzi ya kijeshi, katika mji wa Launglon, Myanmar Aprili 8, 2021. DAWEI WATCH via REUTERS - DAWEI WATCH

Waandamanaji dhidi ya mapinduzi ya kijeshi ya Februari 1 nchini Myanmar wamelipiza kisasi dhidi ya ukandamizaji uliofanywa na vikosi vya usalama katika mji ulioko kaskazini magharibi mwa nchi kwa kutumia bunduki na mabomu wakati wa makabiliano ambapo angalau kumi na moja kati yao wameuawa, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.

Matangazo ya kibiashara

Katika mji wa Taze, magari sita ya vikosi vya usalama mwanzoni yalitumwa dhidi ya waandamanaji, mashirika ya habari ya Myanmar Now na Irrawaddy yamesema.

Magari mengine matano yalikuja kusaidia vikosi vya Myanmar baada ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ya waandamanaji ambao walikuwa wamejihami kwa bunduki, visu na mabomu ya moto, mashirika hayo yameongeza.

Mapigano hayo yameendelea hadi Alhamisi asubuhi na waandamanaji wasiopungua 11 wamepoteza maisha na wengine karibu 20 wamejeruhiwa, mashirika ya habari yameripoti.