URUSI

Jeshi la wanamaji la Urusi laanza mazoezi ya kijeshi katika Bahari Nyeusi

Kikosi cha wanamaji cha Urusi kikifanya mazoezi ya kijesi katika Bahari Nyeusi.
Kikosi cha wanamaji cha Urusi kikifanya mazoezi ya kijesi katika Bahari Nyeusi. REUTERS - SERGEY PIVOVAROV

Jeshi la Wanamaji la Urusi limeanza luteka katika Bahari Nyeusi leo Jumatano kabla ya kuwasili katika ukanda huo meli za kivita za Marekani, mashirika ya habari ya Urusi yameripoti.

Matangazo ya kibiashara

Meli kubwa za kivita za Urusi zimeegeshwa kwenye Bahari Nyeusi upande wa Urusi, zinashiriki katika mazoezi haya ya kijeshi pamoja na ndege za kivita na helikopta. Mazoezi haya yawezesha jeshi la Wanamaji la Urusi kufanya mazoezi ya kupiga risasi adui juu au angani, kulingana na vyombo vya habari.

Meli mbili za kivita za Marekani zinatarajiwa kuwasili katika Bahari Nyeusi baadaye wiki hii wakati Marekani na NATO wanaituhumu Urusi kuendelea kukusanya vikosi vyake kwenye mpaka wake na Ukraine na huko Crimea, jimbo lililounganishwa na Moscow mnamo mwaka 2014.

Urusi imeshauri meli za Marekani kukaa mbali na Crimea "kwa usalama wake" na ikaita kitendo cha Marekani kupeleka majeshi yake kwenye Bahari Nyeusi ni uchochezi.