AZERBAIJAN-ULINZI

Azerbaijan yawashikilia wanajeshi 6 wa Armenia katikati mwa mvutano mkali

Askari wa kabila la Armenia anatazama kupitia darubini akiwa amesimama katika maeneo ya mapigano karibu na kijiji cha Taghavard kilichogawanyika katika mkoa wa Nagorno-Karabakh.
Askari wa kabila la Armenia anatazama kupitia darubini akiwa amesimama katika maeneo ya mapigano karibu na kijiji cha Taghavard kilichogawanyika katika mkoa wa Nagorno-Karabakh. REUTERS - ARTEM MIKRYUKOV

Azerbaijan imewakamata wanajeshi sita wa vikosi vya Armenia Alhamisi hii asubuhi, wizara za ulinzi za nchi hizo mbili zimesema, sehemu ya hivi karibuni ya mivutano ya mipaka iliyoongezeka tangu mwanzoni mwa mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Baku inawashutumu wanajeshi sita wa Armenia kwa kujaribu kuvuka mpaka, wakati Yerevan inadai kwamba wanajeshi wake walikuwa wakifanya kazi ya uhandisi katika eneo la mpaka wa mkoa wa Armenia wa Gegharkunik.

"Hatua zinazohitajika zinachukuliwa kuwarejesha wanajeshi waliotekwa," wizara ya ulinzi ya Armenia imesema.

Kaimu Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pachinian ametaka kutumwa kwa waangalizi wa kimataifa kutoka Urusi au nchi zingine kwenda sehemu ya mkoa wa mpaka na Azerbaijan, ambapo amesema kuna hali ya wasiwasi.

"Ninatoa wito kwa jamii ya kimataifa na pendekezo langu pia linaelekezwa kwa viongozi wa Azerbaijani" amesema, kulingana na taarifa zilizoripotiwa na mashirika ya habari ya Urusi.

"Tukubaliane kwamba vitengo vya jeshi vya kambi hizo mbili huhama haraka kutoka mpakani na kurudi kwenye vituo vyao vya kudumu, na kuweka wachunguzi wa kimataifa kutoka Urusi au nchi zingine za kundi la Minsk", ameongeza Nikol Pachinian, ambaye alijiuzulu mwezi uliopita, chini ya shinikizo kutoka kwa jeshi, kabla ya uchaguzi wa mapema wa Juni 20.

Armenia mwezi huu ilishutumu Azerbaijan kwa kukiuka uhuru wake, ikisisitiza udhaifu wa usitishaji mapigano uliofikiwa chini ya mwavuli wa Urusi mwezi Novemba mwaka uliyopita baada ya wiki kadhaa za mzozo huko Nagorno-Karabakh.

Baku Jumanne ilifutiliambali mashtaka kutoka kwa Yerevan kwamba jeshi lake ilirusha risasi na kuvuka mpaka dhidi ya ngome za jeshi la Armenia.