MAREKANI-CHINA

Marekani kuchukuwa vikwazo dhidi ya maafisa wa China kuhusu Hong Kong

Rais wa Marekani Joe Biden anafanya mkutano wa pande mbili na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, White House, Washington, Julai 15, 2021
Rais wa Marekani Joe Biden anafanya mkutano wa pande mbili na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, White House, Washington, Julai 15, 2021 via REUTERS - Guido Bergmann/Bundesregierung

Marekani inajiandaa kuwachukulia vikwazo maafisa kadhaa wa China leo Ijumaa juu ya suala la kukandamizwa kwa demokrasia huko Hong Kong, na vile vile kuonya makampuni ya kimataifa yanazofanya kazi huko Hong Kong juu ya hali mbaya, kulingana na shirika la habari la REUTERS, likinukuu vyanzo viwili vilivyo karibu na suala hilo.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe saba wa Ofisi ya Uhusiano, chombo cha mamlaka kuu ya China huko Hong Kong, watakabiliwa na vikwazo vya kifedha, vyanzo hivyo vimesema.

Onyo la kibiashara, lililootolewa na Wizara ya mambo ya kigeni, limeelezea wasiwasi wa serikali ya Marekani juu ya athari ya sheria ya usalama wa kitaifa ya Hong Kong kwa biashara za kimataifa. Wakosoaji wanasema Beijing ilitekeleza sheria hiyo mwaka jana kusaidia kukandamiza wanaharakati wanaotetea demokrasia na waandishi wa habari.

"Hali huko Hong Kong inazidi kuwa mbaya. Na serikali ya China inashindwa kutekeleza ahadi iliyotoa juu ya jinsi itakavyoshughulikia mji huo, kwa hivyo hii ni nasaha zaidi juu ya kile kinachoweza kutokea huko Hong Kong, "Joe Biden amesema katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye anazuru Washington.

Hatua hizi, ambazo zitaikera Beijing, ni juhudi za hivi karibuni za utawala wa Biden kuiwajibisha serikali ya China kwa kile Washington inaita mmomomyoko wa sheria katika koloni la zamani la Uinereza ambalo lilirudi chini ya udhibiti wa China mnamo mwaka wa 1997.

Vyanzo hivyo viwili, ambavyo havikupenda kutaja majina yavyo, vimesema hatua za Hong Kong bado zinaweza kubadilika. Chanzo kimoja kimesema kuwa Ikulu ya White House pia inatathmini uwezekano wa sheria ya uhamiaji kutoka Hong Kong, lakini utekelezaji wake bado haujathibitishwa.

Idara ya Fedha ya Marekani ilikataa kujieleza juu ya jambo hilo baada ya vyombo vya habari kuripoti wiki hii juu ya uwezekano wa vikwazo vipya.