INDIA

India: Maporomoko ya udongo yaua thelathini Mumbai

Katika saa 24 zilizopita, mamlaka imerekodi tahadhari 11 kuhusu kuanguka kwa kuta au nyumba katika mkoa wa Mumbai.
Katika saa 24 zilizopita, mamlaka imerekodi tahadhari 11 kuhusu kuanguka kwa kuta au nyumba katika mkoa wa Mumbai. Reuters

Watu wasiopungua 30 wamefariki katika vitongoji vya Mumbai wakati majengo yalipoporomoka kufuatia kuporomoka kwa udongo, hali ambayo ilisababishwa na mvua kubwa, mamlaka imesema.

Matangazo ya kibiashara

Televisheni nchini India zimeonyesha picha za maafisa wa idara ya uokoaji wakisafisha magofu kwa mikono ili kupata miili ya watu waliopoteza maisha, na maafisa wameonya kuwa waathiriwa zaidi wanaweza kukwama katika nyumba zilizoporomoka.

Katika saa 24 zilizopita, mamlaka imerekodi tahadhari 11 kuhusu kuanguka kwa kuta au nyumba katika mkoa wa Mumbai.

Waziri Mkuu Narendra Modi ametoa rambirambi katika ukurasa wake wa Twitter na kuahidi msaada kwa waathiriwa.

Maeneo kadhaa ya jiji yalikumbwa na mafuriko wakati mvua kubwa ziliponyesha saa 24 zilizopita na usafiri ulizorota.

Mvua kubwa inatarajiwa mjini Mumbai na pwani ya viwanda ya jimbo la Maharashtra kwa siku nne zijazo, kulingana na utabiri wa hali ya hewa.

Mvua kubwa, hasa wakati wa msimu wa masika ambao huanza kuanzia mwezi wa Julai hadi Septemba nchini India, husababisha majengo kuporomoka mara kwa mara, hasa makaazi ya zamani na yaliyojengwa kinyume cha sheria.