CHINA

China yakabiliwa na mafuriko makubwa kufuatia mvua zinazonyesha

Wakazi wa Kijiji cha Gongyi, Mkoa wa Henan, wanatembea juu ya daraja lililoporomoka. Julai 21, 2021.
Wakazi wa Kijiji cha Gongyi, Mkoa wa Henan, wanatembea juu ya daraja lililoporomoka. Julai 21, 2021. © REUTERS - China Daily

Makumi ya maelfu ya watu wamehamishwa leo Alhamisi katika maeneo ya katikati mwa China tangu mwanzoni mwa juma hili kufuatia mvua kubwa zinazonyesha ambazo zimesababishavifo vya watu wasiopungua 33 katika mkoa wa Henan.

Matangazo ya kibiashara

Miji mingi imekumbwa na mafuriko na mazao kuharibiwa wakati dhoruba ikielekea kaskazini. Shirika la habari la China linakadiria kuwa China imepoteza yuan bilioni 1.22 (sawa na euro milioni 160).

Watu 12 waliokwama kwenye barabara kuu ya chini ya ardhi katika mji mkuu wa mkoa wa Henan, Zhengzhou, karibu kilomita 650 kusini magharibi mwa Beijing ni miongoni mwa waathiriwa.

Kulingana na shirika la habari la Xinhua, zaidi ya wakaazi 70,000 wa jiji la Anyang, kwenye mpaka kati ya mkoa wa Henan na Hebei, wamehamishwa baada ya mvua kubwa kunyesha tangu Jumatatu.

Jiji la Xinxiang, kaskazini mwa Zhengzhou, limerekodi mvua ya kubwa kati ya Jumanne na leo Alhamisi.

Siku ya Jumatano jioni, hali mbaya ya hewa tayari ilikuwa imeathiri watu 470,000 na hekta 55,000 za mazao, kulingana na hesabu ya Xinhua.