PAKISTANI

Pakistani yakanusha kuhusika kumhifadhi Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Osama Bin Laden

Waziri Mkuu wa Pakistani Yousuf Raza Gilani ambaye ametoa tamko la kifo cha Kiongozi wa Al Qaeda, Osama Bin Laden
Waziri Mkuu wa Pakistani Yousuf Raza Gilani ambaye ametoa tamko la kifo cha Kiongozi wa Al Qaeda, Osama Bin Laden Reuters

Serikali ya Pakistani imekanusha tuhuma za taifa hilo kuhusika kumhifadhi aliyekuwa Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Osama Bin Laden ambaye aliuawa na Makomandoo wa Marekani karibu na Kambi ya Jeshi ya nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya serikali ya Pakistani imetolewa Bungeni na Waziri Mkuu wa taifa hilo Yousuf Raza Gilani ambaye ametumia dakika thelathini kuzungumzia kifo cha Osama Bin Laden.

Waziri Mkuu Gilani amesema kwanza nchi yake haistahili kulaumiwa kwa namna yoyote ile kutokana na kushindwa kugundua Osama alikuwa anaishi katika nchi hiyo kwa miaka mitano.

Kiongozi huyo wa serikali ya Pakistani amesema taifa lake halijawahi kumualika hata mara moja Osama Bina Laden ambaye amekuwa akisakwa kama gaidi namba moja kwa kipindi cha karibu miaka kumi.

Waziri Mkuu Gilani amekwenda mbali na kusema kifo cha Osama hakina maana kama ugaidi umemalizika duniani na badala yake ni kuangalia namna ya kushughulikia matatizo ambayo yanachangia uwepo wa ugaidi.

Tamko hili mbele ya Bunge lililotolewa na Waziri Mkuu Gilani ndiyo la kwanza rasmi kuelezea namna ambavyo operesheni ya kufanikisha kifo cha Osama Bin Laden ilivyofanywa na Makomandoo wa Marekani.

Waziri Mkuu Gilani ameitaka dunia kujiuliza ni kwa nini ilishindwa kutambua kama Osama Bin Laden amekuwa akiishi nchini Pakistani bila ya kuweza kukabiliana naye kwa kipindi cha miaka mitano.

Pakistan Prime Minister Yousuf Raza Gilani On Osama Bin Laden Death

Gilani ameongeza kuwa kama lawama basi inabidi zielekezwe kwa intelijensia ya dunia ambayo kila kukicha imekuwa ikimsaka Osama Bin Laden tangu alipoanza kutekeleza mashambulizi na Mtandao wake wa Al Qaeda.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Gilani amesema ni lazima uchunguzi ufanyike kubaini ni kwa namna gani Osama alifanikiwa kuishi katika taifa hilo bila ya kufahamika.

Serikali ya Pakistani imeongeza kuwa uchunguzi huo utakuja na majibu ya kina nani ambao walikuwa wanamfadhili Osama Bin Laden na kufanikiwa kuishi katika taifa hilo bila ya kutambulika.

Tangu kuuawa kwa Osama Bin Laden tarehe 2 ya mwezi Mei kumekuwa na taarifa nyingi za kukunganya huku Pakistani ikilaumiwa kwa kushindwa kugundua uwepo wake kitu ambacho kimekuwa kikitishia uhusiano wake na Marekani.