THAILAND

Uchaguzi Mkuu nchini Thailand kufanyika mapema mwezi Julai

Waziri Mkuu wa Thailand Abhisit Vejjajiva akiwa na wananchi wa taifa hilo kwenye moja shughuli zake za kijamii
Waziri Mkuu wa Thailand Abhisit Vejjajiva akiwa na wananchi wa taifa hilo kwenye moja shughuli zake za kijamii Reuters

Serikali nchini Thailand imetangaza tarehe 3 ya mwezi Julai ndiyo Uchaguzi Mkuu utafanyika baada ya Mfalme wa nchi hiyo Bhumibol Adulyadej kuridhia ombi la Waziri Mkuu Abhisit Vejjajiva kulivunja bunge.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Serikali ya Thailand Panitan Wattanayagorn amewaambia wanahabari Mfalme wa nchi hiyo amevunja Bunge kuanzia leo na hivyo ni wazi kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu kimeshaanza.

Kwa mujibu wa sheria za Thailand uchaguzi Mkuu unastahili ufanyike katika kipindi cha siku 45 hadi 60 baada ya Mfalme kuvunja Bunge ambalo lilikuwa madarakani.

Uchaguzi huu unakuja ikiwa ni kipindi cha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Jiji la Bangkok kushuhudia mashambulizi makali yaliyoelekezwa kwa wapinzani wa serikali wanaofahamika kama “Red Shirt”.

Watu zaidi ya tisini walipoteza maisha kwenye mashambulizi hayo ambapo wafuasi wa Red Shirt walikuwa wanataka Waziri Mkuu Vejjajiva na serikali yake waondoke madarakani.

Waziri Mkuu wa sasa anatarajiwa kusimama tena kutetea wadhifa wake huku wengi wakiamini uchaguzi huo utakuwa mgumu kwa kuwa unaweza kuleta mshikamano wa taifa au ukauvunja kabisa.

Kinyang'anyiro kinatarajiwa kuwa kikali baina ya Waziri Mkuu Vejjajiva na Mgombea ambaye atateuliwa kutoka Chama cha Waziri Mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra.
Vejjajiva ambaye ni mzaliwa wa Uingereza Chama chake kinaungwa mkono zaidi katika eneo la Bangkok na hata Kusini mwa nchi hiyo lakini kwenye chaguzi zilizopita kimeshindwa kushindwa na kujikuta kwenye hali ngumu.