Mgomo wa wafanyakazi nchini Ugiriki watikisa sekta ya usafiri
Imechapishwa: Imehaririwa:
Maelfu ya wananchi nchini Ugiriki wameanza mgomo ambao umeathiri sekta nyingi na kuchangia kukosekana kwa usafiri wakionesha hasira zao kutokana na hatua ambazi zinachukuliwa na serikali katika kukabiliana na deni ambalo linaikabili nchi hiyo.
Wafanyakazi wa Sekta ya Umma wanaokadiriwa kufikia 20,000 wameandamana katika Miji ya Athens na Thessaloniki wakidai hawaridhishwi na hatua ya kutaka kuachishwa kazi mara kwa mara kwa sababu ya deni kubwa linaloikabili serikali.
Serikali imelazimika kufanya mabadiliko ya ushuru huku wakilipa mishahara midogo kwa wafanyakazi lengo likiwa ni kupunguza matumizi ili pesa nyingine itumike kufidia deni ambalo Ugiriki inadaiwa.
Wafanyakazi hao wameituhumu serikali imechangia hali ya uchumi kuwa mbaya kutokana na kuwa na sera mbovu za kiuchumi ambazo zimeifanya kukopa dola bilioni 158 kutoka Umoja wa Ulaya EU na Shirika la Fedha Duniani IMF.
Polisi ambao wanashika doria katika Jiji la Athens wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamebeba mawe na kuzingira Bunge la nchi hiyo.
Taarifa za polisi zimedokeza watu saba wamejeruhiwa huku wengine watano wakishikiliwa kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kuhusika kwenye ghasia hizo.
Mkuu wa Umoja wa Wafanyakazi nchini Ugiriki GSEE Yiannis Panagopoulos ametoa taarifa ambayo inalaani mipango ya serikali kwa kuwa imekuwa haiwatendei haki wafanyakazi wa taifa hilo.
Panagopoulos ameongeza kuwa wamechukizwa kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana wamefikia uamuzi wa kuandamana kuonesha namna wanavyochukizwa na sera za serikali.
Wafanyakazi ambao wameandamana na kuchangia kusitishwa kwa safari za ndege za ndani na nje wamejiapiza kutokuwa tayari kushuhudia ukandamizaji unaofanywa na serikali dhidi yao.
Hii si mara ya kwanza kwa wafanyakazi nchini Ugiriki kugoma kutokana na sera mbaya za nchi hiyo ambayo inakabiliwa na deni kubwa baada ya kuchukua mkopo kutoka EU na IMF baada ya kutetereka kiuchumi.