LIBYA

NATO yakana mashambulizi yao nchini Libya yanalengo la kumuua Kanali Muammar Gaddafi

Waasi wakifanya mazoezi ya kivita katika Mji wa Benghazi eneo ambalo ni kambi yao kwa sasa
Waasi wakifanya mazoezi ya kivita katika Mji wa Benghazi eneo ambalo ni kambi yao kwa sasa Reuters

Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO yameendelea kusisitiza shambulizi ambalo walilifanya nchini Libya halikuwa na lengo la kumuua Kiongozi wa Taifa hilo Kanali Muammar Gaddafi.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya NATO imekuja wakati ambapo Waasi wakitangaza kusonga mbele katika Jiji la Misurata na kuvirudisha nyuma vikosi vya Kanali Gaddafi ambavyo vinahaha kulirudisha eneo hilo kwenye himaya yake.

Brigedia Jenerali Claudio Gabellini amewaambia wanahabari kuwa tangu wameanza mashambulizi yao nchini Libya tarehe 31 ya mwezi March wamekuwa na jukumu moja kubwa la kulinda wananchi.

Kiongozi huyo wa Kijeshi ameongeza kuwa mashambulizi yote ambayo yanafanywa na Majeshi ya NATO yanawalenga wanajeshi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwashambulia wananchi na si vingine.

Brigedia Jenerali Gabellini akizungumza kutoka Nepal ameweka bayana hawana mpango wa kuwashambulia wananchi na hakuna ushahidi kama mashambulizi yao yalilenga kumuua Kanali Gaddafi.

Tamko hilo na Majeshi ya NATO yanakuja wakati Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Anders Fogh Rasmussen akiwa amenukuliwa akisema muda wa Kanali Gaddafi kuendelea kusalia madarakani unahesabika.

Katika shambulizi lililofanyika tarehe 1 mwezi May lilisababisha kifo cha mtoto wa pili wa Kabali Gaddafi, Seif Al Arab pamoja na wajukuu zake watatu ambao walikuwa kwenye nyumba iliyoshambuliwa.

Naye Kiongozi wa Waasi nchini Libya Mahmud Jibril anatarajiwa kukutana na Wabunge wa Bunge la Marekani kujadili hali ilivyo katika nchi yake ambayo imeshuhudia machafuko yaliyosababisha maelfu ya wananchi kupoteza maisha huku wengine laki saba na elfu hamsini wakikimbia makazi yao.

Nazo taarifa za karibuni zinaeleza waasi wamefanikiwa kuwadhibiti wanajeshi wa Kanali Gaddafi katika Uwanja wa Ndege wa Misurata ambapo mashuhuda wanasema milio ya risasi imesikika.

Umoja wa Ulaya EU nao kupitia Mkuu wake wa Masuala ya Sera za Kimataifa Catherine Ashton unajiandaa kufungua ofisi katika Mji wa Benghazi ili kudhihirisha unatambua Mamlaka inayoongoza eneo hilo.