LIBYA

Mashambulizi ya Majeshi ya NATO nchini Libya yaua watu sita

Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi katika moja ya hotuba zake kwa wananchi wa taifa hilo
Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi katika moja ya hotuba zake kwa wananchi wa taifa hilo © REUTERS

Mashambulizi ya angani ya Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO yaliyotekelezwa siku ya Alhamisi kulenga makazi ya Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi yamesababisha vifo vya watu sita wakati huu Waasi wakishangilia kutwaa Uwanja wa Ndege wa Misurata.

Matangazo ya kibiashara

Utawala wa Libya umethibitisha vifo hivyo huku watu wengine 10 wakijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ambayo ni ya tatu kulenga makazi ya kanali Gaddafi tangu NATO waanze kuwasaidia Waasi.

Mashambulizi haya yamekuja saa moja baada ya Kanali Gaddafi kuonekana kwa mara ya kwanza akiwa amekutana na Viongozi wa Kijadi ambao walikuwa na mazungumzo naye kwenye Ikulu ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wanasema Ndege za Kijeshi za NATO zilifanya mashambulizi manne katika kipindi cha saa moja na kufanikisha vifo hivyo katika Mji Mkuu Tripoli.

Shambulizi hili linakuja wakati ambapo Waasi wametoa mwaliko kwa serikali ya Uingereza kwenda kufungua Ubalozi wao katika Jiji la Misurata baada ya kufanikiwa kuutwaa Uwanja wa Ndege.

Mapema siku ya Alhamisi Televisheni ya Taifa ya Libya imeonesha picha za mkutano wa Kanali Gaddafi akiwa amekutana na Viongozi wa Kijadi kutoka eneo lenye Waasi kwa mara ya kwanza.

NATO wameshatoa taarifa ambayo inaeleza shambulizi lao lilikuwa na lengo la kuwalinda wananchi na si kumuua Kanali Gaddafi kama ambavyo inaelezwa na serikali yake.

Huko nchini Uingereza katika Jiji la London Kiongozi wa Waasi Mustafa Abdul Jalil amekutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu David Cameron baada ya wao kufanikiwa kuuweka kwenye himaya yao Uwanja wa Ndege wa Misurata.

Waziri Mkuu Cameron amemhaidi Kiongozi huyo wa waasi kwamba nchi yake ipo tayari kuwapa msaada hata wa kidiplomasia katika Jiji la Benghazi ambapo wanautawala kamili.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akizungumzia hali inavyoendelea Libya

Cameron hakusita kumwambia Kiongozi huyo wa Waasi kwamba wanawakaribisha wafungue Ubalozi wao nchini Uingereza kutokana na nchi hiyo kuutambua utawala wao.

Tatizo kubwa kwa sasa nchini Libya limekuwa ni mahitaji ya kibinadamu kwa mamia ya wananchi ambao wanateseka kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya Jeshi la Kanali Gaddafi dhidi ya Waasi wanaopewa nguvu na Majeshi ya NATO.

Tayari Shirika la Chakula Duniani WFP limetaka mapigano yasitishwe katika Miji ya Misurata na Magharibi mwa taifa hilo ili waweze kufikisha misaada kwa maelfu ya wananchi waohitaji chakula na matibabu.