AFGHANISTAN

Mashambulizi ya NATO yaua watu 14 nchini Afghanistan

Watoto wa shule wakipita katika kambi moja ya vikosi vya NATO kusini mwa nchi ya Afghanistan
Watoto wa shule wakipita katika kambi moja ya vikosi vya NATO kusini mwa nchi ya Afghanistan Reuters

Watu kumi na nne wamekufa na wengine zaidi ya Ishirini wamejeruhiwa kusini mwa jimbo la Helmand nchini Afghanistan kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na vikosi vya majeshi ya NATO . 

Matangazo ya kibiashara

Gavana wa jimbo la Helmand amesema kuwa mashambulizi hayo ya vikosi vya NATO yalifanywa kufuatia vikosi vya serikali vilivyoko katika mji huo kuomba msaada kutoka kwa majeshi ya NATO kufuatia vikosi hivyo kuvamiwa na wanamgambo wa Taliban na kuanza kuahsmbuliwa.

Gavana huyo ameongeza kuwa shambulio hilo limeua watoto 12 na raia wengine wawili katika shambulio ambalo amelielezea kuwa ni la bahati mbaya kutokana na vikosi vya NATO kupokea taarifa tofauti toka kwa makamanda wa vikosi vya Afghanistan.

Nae mseamji wa vikosi hivyo vya umoja vya ISAF nchini humo amesema kuwa mara baada ya kufanya mashambulizi usiku wa kuamkia leo nao pia wamepeleka wataalamu wao katika eneo hilo kuchunguza ili kudhibitisha taarifa za kuuawa kwa raia wasio na hatia.

Mara kadhaa serikali ya Afghanistan imekuwa ikiingia katika mgogoro na majeshi ya NATO kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanyika kimakosa na vikosi hivyo kwa kuwaua raia wasio na hatia.

Wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan wameapa kuendelea na mashambulizi zaidi waliyodai yanalenga kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa kiongozi wa Al Qaeda Osama Bin Laden.