INDIA

Hatukuwa na njia nyingine zaidi ya kutumia nguvu: Manmohan Singh

Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh
Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh Reuters

Waziri mkuu wa India Manmohan Singh amesema polisi hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kuwatawanya maelfu ya wafuasi wa Guru Baba Ramdev waliokuwa wamekusanyika katika mji wa delhi kushinikiza serikali kupitisha sheria mpya ya kushughulikia wala rushwa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa upande mwingine waziri mkuu huyo amesema kuwa kitendo cha polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya wafuasi wa Guru haikuwa sahihi sana lakini kwa upande mwingine ilikuwa ni lazima watekeleze walichokifanya.

Baba Ramdev wikiendi hii alitangaza kuanza mgomo wa kutokula mpaka pale serikali ya waziri mkuu Singh itakapopitisha sheria ya kunyongwa kwa viongozi na watu ambao watapatikana na hatia ya kushiriki vitendo vya rushwa.

Kabla ya kuanza kwa mgomo wake huo, kiongozi huyo aliwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika mji wa delhi akisema kuwa amechoshwa kuishi kwenye nchi ambayo imeshamiri vitendo vya rushwa na kuwa anaimani kitendo cahe cha kuamua kutokula mpaka kufa kutasaidia kuishawishi serikali kuharakisha upitishwaji wa sheria hiyo.

Zaidi ya watu 30 walijeruhiwa katika mapambano kati ya wafuasi wa Guru Ramdev na polisi ambao walilazimika kuingilia kati umati wa watu ambao walikuwa wakiandamana kushinikiza serikali kuwabana wala rushwa.

Wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na wanasheria nchini India wamelaani vikali mashambulizi ambayo yamefanywa na polisi dhidi ya mkusanyiko waliouita wa amani uliofanywa na kiongozi huyo kwa lengi la kuikumbusha serikali majukumu yake katika kupambana na wala rushwa.

Wakati huohuo mahakama kuu nchini humo imeagiza serikali kupitia kwa waziri mkuu Sighn kutoa taarifa kwa kile ambacho kilitokea na kiufanywa na polisi kwa kuwatawanya wafuasi wa guru Ramdev ambao walikuwa wamekusanyika kwa amani kushinikiza serikali kupambana na wala rushwa.

Akizungumza akiwa nyumbani kwake mjini Haridwar baba Ramdev ameapa kuendelea na mgomo wake mpaka pale serikali itakaposikiliza kilio chake.

Serikali ya waziri mkuu Manmohan Singh imekuwa ikishutumiwa kwa kuwakumbatia viongozi wala rushwa huku wacahmbuzi wa mambo wakisema kuwa kushuka kwa uchumi wa nchi hiyo na kupanda kwa gharama za maisha kumetokana na viongozi hao kujilimbikizia mali.