ICC-OCAMPO

Ocampo kufungua mashtaka mapya dhidi ya Kanali Moamer Gaddafi

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya ICC,  Luis Moreno-Ocampo
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya ICC, Luis Moreno-Ocampo Reuters/Jerry Lampen

Kwa mara nyingine tena mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya ICC Luis Moreno Ocampo ameibuka tena jumatano hii na kutangaza kuanzisha uchunguzi mpya dhidi ya kanali Moamer Gaddafi kuamuru wanajeshi wake kufanya vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake nchini mwake.

Matangazo ya kibiashara

Mwendesha mashtaka huyo amesema kuwa hivi sasa anasubiri uamuzi wa awali wa majaji kuhusiana na kutolewa kwa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya Kanali Gaddaf na wenzake wawili ndipo atawasilisha tena ombi la mashtaka ya ubakaji dhidi ya kiongozi huyo.

Ocampo ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa na kusema kuwa ofisi yake imeendelea kuapata ushahidi mpya unaoonyesha askari wa kiongozi huyo wakifanya vitendo vya ubakaji katika miji ya Misrata na miji mingine ambayo walivamia.

Ameongeza kuwa uchunguzi wa awali wa ofisi yake umebaini kuwa wanajeshi hao wanafanya vitendo hivyo kwa kuwa wamepatiwa dawa za kuongeza vichocheo vya kufanya vitendo hivyo na kiongozi wao.

Amesema kuwa vidonge hivyo ni sehemu ya mkakati wa kanali Gaddafi kuhakikisha kuwa anawatishia wananchi hususani wanawake kutoshirikiana na wapiganaji waasi ambao wamekuwa wakiipinga serikali yake kwa vitendo vya unyanyasaji.

Bwana Ocampo amesema kuwa anaimani kubwa mara baada ya kutolewa kwa maamuzi ya majiji kuhusiana na mashtaka ya awali basi atawasilisha mashtaka hayo mapya ambayo pia anaamini majaji watakubalina nayo na kumfungulia mashtaka mapya ubakaji kiongozi huyo wa Libya.

Hatua ya kufunguliwa kwa mashtaka hayo mapya ya ubakaji dhidi ya kiongozi huyo wa Libya yamekuja kufuatia kisa cha mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Iman a-Obeid ambaye mwezi march aliripoti kufanyiwa visa vya ubakaji na askari wa Gaddaf ambapo alikamatwa na kufanikiwa kutoroka na sasa yupo katika kambi ya wakimbizi nchini Romania.

Mwendesha mashtaka huyo mwezi mmoja uliopita aliwasilisha ombi la kutolewa kwa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya Moamer Gaddafi, mtoto wake Seif al-Islam na mkuu wa usalama wa taifa Abdullah al-Sanussi.

Wakati huo huo bwana Ocampo amesema anaandaa ushahidi kuhusiana na rais wa Syria Bashar al-Asaad kutokana na kubainika kuamuru wanajeshi wake kuwaua raia wasio na hatia pamoja na kukiuka haki za binadamu.

Kuhusiana na Syria bwana Ocampo amesema pindi atakapomaliza kukusanya ushahidi dhidi ya serikali ya Syria atawasilisha kwa majaji kwa hatua zaidi.