SYRIA

Serikali ya Syria yapeleka wanajeshi zaidi katika mji wa Jisr al-Shughour

Baadhi ya wananchi wa Syria wakivuka mpaka kuingia nchini Uturuki
Baadhi ya wananchi wa Syria wakivuka mpaka kuingia nchini Uturuki Reuters/Anatolian/Ismihan Ozguven

Televisheni ya taifa nchini Syria hii leo imeripoti kuwa vikosi vya jeshi la serikali vimepelekwa katika mji wa Jisr al-Shughour na kuuzunguka mji huo kwa lengo la kurejesha hali ya utulivu katika mji huo.

Matangazo ya kibiashara

Mapema juma hili serikali ya Syria kupitia kwa waziri wa habari ilisema kuwa zaidi ya askari wake 120 waliuawa katika mji huo na waandamanaji ambao sasa wameanza kutumia silha kuwashambulia askari.

Kufuatia tangazo la serikali kuviagiza vikosi vyake kuingia kwa nguvu katika mji huo, tayari wimbi la wakimbizi toka nchini humo kuingia nchi jirani ya Uturuki kuomba hifadhi.

Leo asubuhi waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameushutumu vikali utawala wa rais Bashar al-Asaad akisema kuwa hauko imara katika kuhakikisha inawalinda wananchi wake ili kupunguza wimbi la wakimbizi.

Waziri mkuu huyo ameongeza kuwa kuongezeka huko kwa wananchi toka nchini Syria kunaashiria kuwa hali ya mambo sio shwari na kwamba huenda kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na polisi ndio maana wananchi wamekuwa wakiikimbia nchi yao.

Serikali ya Uturuki imesema kuwa mpaka sasa nchi yake imewapokea zaidi ya wakimbizi elfu mbili ambao wameingia nchini humo na kuongeza kuwa idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mara kutokana na kuendelea kwa operesheni za kijeshi.

Operesheni hiyo ya kijeshi ambayo imeanza kutekelezwa, inalenga kuwasaka viongozi wa vikundi vya watu wenye silaha katika mji wa Jisr al-Shghour ambo serikali imesema ndio wanaoshambulia polisi huku kukiwa na taarifa pia kuna wanajeshi walioasi.

Serikali ya Syria hivi sasa imepiga marufuku kuingia kwa waandishi wa habari wa kimataifa toka vituo vikubwa vya televisheni ikisema kuwa wamekuwa chanzo cha kupotosha ukweli wa mambo ulivyo nchini humo.

Wakati hayo yakiendelea bado baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeendelea kuvutana kuhusiana na hatua ambazo zinafaa kuchukuliwa dhidi ya Syria ili kukomesha mauaji huku nchini za China na Urusi zikiweka wazi kuwa hazitapiga kura ya Turufu kupitisha maazimio yoyote kuhusu nchi hiyo.