ETHIOPIA-ADDIS ABABA

Marais wa Sudan Kusini na Kaskazi kukutana mjini Addis Ababa Ethiopia

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (kushoto) akiwa na rais wa Sudan kaskazini Omar Hassan el-Bashir walipokutana hivi karibuni
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (kushoto) akiwa na rais wa Sudan kaskazini Omar Hassan el-Bashir walipokutana hivi karibuni Reuters

Marais wa Sudan kusini na sudan Kaskazini wanatarajia kukutana na kufanya mazungumzo jumapili hii mjini Addis Ababa Ethiopia mazungumzo yanayolenga kumaliza tofauti zao katika jimbo la Abyei na Kordofan.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa afrika Au, umeonesha kuwa rais Omary Hassan al-Bashiri wa sudan Kaskazini na Salva Kiir wa Sudan kusini kwa pamoja watakutana na rais wa zamani wa afrika kusini Thabo Mbeki ambaye ameteuliwa kushughulikia mzozo huo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa katika mkutano huo utakaofanyika baadae leo hii unatarajiwa kumjumuisha waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi ambaye awali alinukuliwa akisema kuwa anamatumaini kikao hicho kitatoka na jibu.

Taarifa ya umoja huo imesema kuwa ajenda kubwa katika kikao hicho itakuwa ni mgogoro unaoendelea baina ya nchi hizo mbili kuhusiana na jimbo la Abyei na Kordofan ambayo kwa pamoja yana utajiri wa mafuta.

Kikao hicho kinafanyika wakati huu ambapo nchi ya sudan kusini inatarajiwa kutangazwa kwama taifa huru mnamo tarehe 9 ya mwezi julai kufuatia kura ya maoni iliyopigwa mwezi January mwaka huu na wananchi wengi kuonyesha kutaka nchi hizo kujitenga.

Majuma mawili yaliyopita serikali ya sudan Kaskazini kupitia kwa rais wake Hassan al-Bashir ilituma vikosi vyake kushambulia eneo la abyei na kordofan na kuyaweka maeneo hayo mawili katika himaya yake.

Rais Bashir mara kadhaa amenukuliwa akiendelea kusisitiza msimamo wan chi yake kuwa eneo la abyei ni jimbo halali la sudan kaskazini na sio vinginevyo, kauli ambayo inapingana na azimio la baraza la usalam la umoja wa mataifa UN lililoagiza kuondolewa kwa vikosi hivyo.

Siku ya ijumaa vikosi vya sudan kaskazini viliendelea kushambulia miji ya kusini mwa nchi hiyo ambapo walishambulia mji wa Kordofan ambao umekuwa katika machafuko ya muda mrefu ya kimipaka na Sudan Kusini.

Mbali na kujadili migogoro katika majimbo hayo viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia hatma ya kiusalama kati ya mataifa yao pale sudan Kusini itakapotangazwa rasmi kama taifa huru.