Marekani

Marekani yatangaza kumsaka kiongozi mpya wa Alqaeta Al Zawahiri

Kiongozi mpya wa Alqaeda anaetafutwa na Marekani
Kiongozi mpya wa Alqaeda anaetafutwa na Marekani REUTERS/Social Media Website via Reuters TV

Marekani inasema itamtafuta kwa udi na uvumba kiongozi mpya wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri kama walivyofanya kwa Osama Bin Laden.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa juu wa kijeshi nchini humo Mike Mullen amesema al-Qaeda bado ni tishio kubwa kwa usalama wa Marekani, licha ya kuuawa kwa Osama Bin Laden, na kuongeza kuwa Marekani itatumia na inatumia mbinu zote kumsaka AL-Zawahiri.

Ayman al-Zawahiri alitangazwa jana kuwa kiongozi mpya wa mtandao wa al-Qaeda. Tangazo ambalo lilitolewa kupitia tovuti inayotumiwa na makundi ya Kiislamu.  Al-Zawahiri alikuwa mtu wa pili katika uongozi wa mtandao wa Al-Qaeda, anamrithi Osama bin-Laden, alieuawa nchini Pakistan, wiki sita zilizopita na kikosi maalum cha marekani.

Zawahiri mwenye miaka 60 anahesabika miongoni mwa viongozi waliopanga mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 pamoja na mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania. Marekani imeweka zawadi ya dola milioni 25 kwa habari zitakazosaidia kumkamata Zawahiri.

Zawahiri ndie ambae atapanga na kuongoza shughuli zote za mtandao huo wa kigaidi wa  Al-Qaeda.