ZAMBIA-CHILUBA

Rais wa zamani wa Zambia Frederick Chiluba afariki dunia

Raisi wa zamani wa Zambia, Frederick Chiluba
Raisi wa zamani wa Zambia, Frederick Chiluba AFP PHOTO / THOMAS NSAMA

Rais wa zamani wa Zambia Frederik Chiluba amefariki dunia asubuhi ya hii leo nyumbani kwake mjini Lusaka, msemaji wake Emmanuel Mwamba amedhibitisha taarifa hizo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa rais huyo amesema kuwa rais Chiluba kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa kwa matatizo ya moyo na figo ambayo ndiyo yamepelekea kifo chake.

Rais Chiluba aliingia madarakani mnamo mwaka 1991 wakati wa mfumo wa vyama vingi kupitia chama cha Movement for Multiparty Party Democracy ambapo aliiongoza nchi hiyo hadi mwaka 2001 alipoachia madaraka.

Rais Chiluba aliingia madarakani mwaka 1991 katika uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi akichukua madaraka hayo toka kwa rais Kenneth kaunda aliyemkosoa kwa sera zake za kushindwa kukuza uchumi wa taifa hilo.

Mara baada ya kuingia madarakani rais Chiluba alibinafsisha zaidi ya makampuni 250 ya serikali hatua iliyokosolewa vikali na wapinzani wake ambao baadae aliwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Aling'atuka madarakani mwaka 2001 baada ya kushindwa jaribio lake la kutaka kubadili katiba ya nchi hiyo na kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mitatu na hatimaye kumpisha marehemu rais Levy Mwanawasa ambaye alimfungulia mashtaka ya rushwa kiongozi huyo na kupatikana na hatia.

Mwaka 2007 mahakama kuu nchini Uingereza ilitangaza kuzuia mali zote za kiongozi huyo wa zamani wa Zambia zilizokuwa na thamani ya zaidi ya dola za marekani bilioni 4.

Akiwa madarakani rais Chiluba pia aliweza kushinda jaribio la kutaka kupinduliwa mwaka 1996 na wanajeshi waasi ambapo aliwakamata viongozi kadhaa wa upinzani akiwemo kenneth kaunda na baadhi ya waandishi wa habari akiwashutumu kuhusika na upangaji njama wa kufanya mapinduzi.

Rais Chiluba alizaliwa mnamo tarehe 30 ya mwezi wa nne mwaka 1942 ambapo ameacha watoto tisa kwa mke wake aliyeachana nae mwaka 2002 Vera Tambo.