UBELGIJI-UGIRIKI

Mawaziri wa Fedha wa Umoja wa Ulaya EU waahirisha kupitisha msaada wa fedha kwa nchi ya Ugiriki

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou.
Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou. Reuters/Grigoris Siamidis

Mawaziri wa fedha kutoka Umoja wa Ulaya EU, kwa mara nyingine tena wameahirisha kupitisha kiasi cha dola za marekani bilioni 17 saba kwa nchi ya Ugiriki ili kuisaidia nchi hiyo kuondokana na mgogoro wa kifedha unaoikabili nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Katika mkutano wao uliofanyika mjini Luxembourg nchini Ubelgiji, mawaziri hao wa fedha wameshindwa kukubaliana kuhusu kupitisha nyongeza ya msaada wa fedha toka katika umoja huo wa dola bilooni 17 kwa nchi Ugiriki ambayo iliomba kuongezewa mkopo huo.

Badala yake mawaziri hao wa fedha wametoea muda zaidi kwa nchi ya Ugiriki kukubaliana na masharti mapya ya Umoja wa Ulaya yanayoitaka nchi hiyo kuendelea kupunguza matumizi ya fedha na kupunguza wafanyakazi ili kukabilina na mgogoro wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo.

Msaada huo mpya wa kifedha kwa nchi ya Ugiriki unatarajiwa kutolewa na Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Fedha Duniani IMF ambao wote kwa pamoja wameitaka nchi ya Ugiriki kuendelea kufanya mabadiliko mfumo wake wa uchumi pamoja na ajira ili kuweza kupata mkopo huo.

Waziri wa fedha wa Ubelgiji Didier Reynders mara baada ya mkutano huo, amesema kuwa mawaziri hao hawawezi kupitisha kiasi hicho kipya cha fedha bila kupata uhakika kama bunge la Ugiriki litakubalina na mpango mpya uliowasilishwa na waziri mkuu George Papandreou ili kuiwezesha nchi hiyo kuweza kupatiwa fedha hizo.

Tayari Bunge la Ugiriki limeanza kikao chake cha siku tatu hii leo kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na waziri mkuu kabla ya kuyapitisha ama kuyakataa mapendekezo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa ni shinikizo toka Umoja wa Ulaya EU.

Wakati kikao cha Bunge kikiendelea mjini Athens, maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza katika miji mbalimbali wakipinga mpango wa waziri mkuu Papandreou ambapo juma lililopita kulishuhudiwa vurugu kubwa baina ya Polisi na waandamanaji wanaopinga nchi hiyo kuendelea kusaidiwa na umoja wa Ulaya.