UGIRIKI

Waziri mkuu wa Ugiriki ashinda kura ya kuwa na imani nae

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou akihutubia bunge la nchi hiyo
Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou akihutubia bunge la nchi hiyo Reuters/Yiorgos Karahalis

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou hatimaye ameshinda kura ya kuwa na Imani nae iliyopigwa na Bunge la nchi hiyo jana usiku na kumuwezesha kuendelea kusalia madarakani ikiwa ni ishara ya wabunge kukubali mpango wake wa kuiwezesha nchi yake kupata mkopo toka umoja wa Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Wabunge waliopiga kura walikuwa ni 155 ambapo waziri mkuu Papandreou alipata kura 143 huku wabunge wawili wakiwa hawajapiga kura kutokana na kutokuwepo bungeni.

Awali kabla ya kupigwa kwa kura hiyo maelfu ya wananchi walijikusanya nje ya ukumbi wa bunge la nchi hiyo katika mji wa Athens wakiwa na mabango ya kukejeli mpango wa waziri mkuu wao wa kutaka kuongeza kodi na kupunguza bajeti ya serikali kwa kupunguza wafanyakazi.

Kufuatia matokeo hayo ambayo yamemwezesha waziri mkuu Papandreou kusalia madarakani, hivi sasa wabunge wanasubiriwa kupitisha kiasi cha euro bilioni 28 kama kiwango ambacho waziri mkuu wao alikiweka katika kuongeza kodi na kupunguza matumizi mengine ya serikali kukabilina na hali ngumu ya uchumi iliyoikumba nchi hiyo.

Jumatatu wiki hii mawaziri wa fedha wa umoja wa Ulaya walishindwa kukubalina kupitisha msaada wa kifedha wa zaidi ya Euro bilioni 12 kwa nchi ya Ugiriki ikiwa ni awamu ya pili ya mkopo wake kwa nchi ya Ugiriki kama ilivyoombwa na waziri mkuu Papandreou.

Mawaziri hao kwa kauli moja walikubalina kusitisha mpango huo, ili kuruhusu bunge la nchi hiyo kupiga kura endapo watakubaliana na mpango wa serikali ama kuupinga jambo ambalo lingepelekea kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya.

Akiongea mara baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura waziri mkuu Papandreou aliwashukuru wabunge kwa kuonyesha kuwa na imani na serikali yake huku pia akiwapongeza baadhi ya viongozi wa upinzani ambao nao walimpigia kura ya kuwa na imani nae.

Katika hotuba yake pia, waziri mkuu aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati huu ambapo amesema anauhakika kupitia Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha Duniani watapitisha kiasi cha fedha ambacho nchi hiyo ilikiomba ili kuiwezesha kukabiliana na hali mbaya ya kifedha iliyoikumba nchi hiyo.

Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya sasa wanasubiriwa kuketi tena juma lijalo kupitisha kiwango cha fedha ambacho kiliombwa na nchi ya Ugiriki.