Libya-Tripoli

Kiongozi wa Libya avitwika lawama vikosi vya NATO kwa kuendesha mauaji ya raia nchini mwake

Kiongozi wa libya Muamar Gadaffi
Kiongozi wa libya Muamar Gadaffi ©Reuters

Kiongozi wa Libya kanali Muammar Gaddafi ameyalaumu majeshi ya kujihami ya umoja wa nchi za magharibi, NATO kwa mauaji ya raia yanayotekelezwa nchini mwake na majeshi ya NATO.  

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Gaddafi imekuja baada ya NATO kufanya mashambulizi mfululizo na kuua raia wakiwemo watu wa familia ya msaidizi wake wa karibu na amesema vitendo hivyo ni kinyume na haki za binadamu.

Gaddafi amesema kuwa vitendo vinavyofanywa na NATO havitawazuia wao kupambana mpaka dakika ya mwisho na wako tayari kufa katika kukabiliana na vitendo hivyo.

Kiongozi huyo wa Libya amesema kuwa mashambulizi ya NATO ni haramu na wanaoshiriki kuua watu wa Libya ni wahalifu wanaolenga kuiangamiza Libya na watu wake.

Majeshi ya NATO yamekiri kuhusika na baadhi ya vifo vya raia lakini hayawalengi raia moja kwa moja kama inavyodaiwa na serikali ya Muammar Gadaffi.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Italia imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia watu walioathirika na vita.