Ufaransa-Afghnistani

Ufaransa nayo yatangaza kuviondowa vikosi vyake nchini Afghanistani sambamba na vile vya Marekani

Reuters/Philippe Wojazer

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ametangaza hatua ya kuondoa wanajeshi wa nchi yake wapatao elfu nne wanaoshika doria nchini Afghanistan ikiwa ni kufuata kile ambacho kimeamualiwa na Rais wa Marekani Barack Obama.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye taarifa ambayo imetolewa na Ikulu ya Ufaransa imesema wanaunga mkono hatua iliyochukuliwa na Marekani ambayo Rais wake ametangaza kuondoa wanajeshi elfu thelathini na tatu katika kipindi cha miezi kumi na tano.

Hatua ya kuondolewa kwa majeshi hayo kumepokelewa kwa mitizamo tofauti kwani Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amepongeza hatua hiyo huku Seneta wa Republican John McCain akisema hatua hiyo imefanywa kwa haraka.

Kwa upande wao Wanamgambo wa Taliban wamesema muda huo ni mwingi sana kwa majeshi hayo kuondoka huku Mpinzani wa Rais Karzai, Dokta Abdullah Abdullah akisema huu ni wakati wa kufanyika kwa mabadiliko kabla ya mwaka 2014.

Tayari nchi za Uingereza, Ujerumani na Australia ambazo zina wanajeshi wake zimejitokeza na kuunga mkono uamuzi wa kuondolewa kwa vikosi hivyo nchini Afghanistan kwa kipindi cha miezi kumi na tano.