UGIRIKI

Maandamano zaidi yaendelea nchini Ugiriki

Polisi wakipambana na waandamanaji mjini Athens, Ugiriki
Polisi wakipambana na waandamanaji mjini Athens, Ugiriki Reuters

Hali ya usalama nchini Ugiriki imeendelea kuwa tete kufuatia kuendelea kwa mapambano baina ya Polisi na waandamanaji katika mji mkuu wa nchi hiyo Athens wakipinga hatua ya serikali kukubali masharti ya Umoja wa Ulaya EU na Shirika la Fedha Duniani IMF.

Matangazo ya kibiashara

Maofisa usalama nchini Ugiriki wamesema kuwa zaidi ya watu 46 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo ya nchi nzima yaliyoitishwa na shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini humo kushinikiza bunge kutokubali mapendekezo ya serikali.

Vurugu hizo zinaendelea wakati ambapo muda mchache ujao bunge la nchi hiyo litakutana kupiga kura ya kukubali amba kukataa mapendekezo ya serikali ya kutaka kuongeza kodi na kubana matumizi ili kukabilina na hali mbaya ya uchumi.

Waziri mkuu wa nchini hiyo George Papandreou amesema kuwa nchi hiyo itakuwa haina fedha zozote ndani ya wiki chache zijazo endapo wabunge hawatapitisha mapendekezo aliyowasilisha majuma kadhaa yaliyopita ili kuiwezesha nchi hiyo kupata msaada wa fedha wa Euro bilioni 28 toka Umoja wa Ulaya na Shirika la fedha duniani IMF.

Endapo bunge la nchi hiyo litapitisha mapendekezo ya serikali basi ni wazi kutatoa nafasi kwa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya kukutana na kupitisha kiasi kingine cha fedha kwa nchi hiyo cha zaidi ya Euro bilioni 120 kama awamu ya pili ya mkopo ambayo nchi hiyo iliomba.

Tayari mkurugenzi mpya wa shirika hilo Christine Lagarde amesema kuwa ili nchi ya Ugiriki iweze kuondoka katika mgogoro ulionao kwa sasa ni lazima wabunge wa pande zote mbili wakubaliane kupitisha mapendekezo ya serikali ya kubana matumizi yatakayowezesha nchi hiyo kupatiwa fedha.

Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini humo siku ya jumanne lilitisha mgomo wa saa 48 kwa nchi nzima kupinga mapendekezo ya serikali wakidai kuwa utaiingiza nchi hiyo katika mzigo mkubwa wa madeni utakaochukua muda mrefu kuweza kulipa.