MAREKANI

Strauss-Kahn aachiwa huru toka kifungo cha Nyumbani

Dominique Strauss-Khan, lors de sa comparution le 6 juin 2011.
Dominique Strauss-Khan, lors de sa comparution le 6 juin 2011. © Reuters

Mahakama ya mjini New York Marekani inayosikiliza kesi dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Fedha Duniani, Dominique Strauss-Kahn imetangaza kumuachia toka katika kifungo cha ndani bosi huyo wa zamani wa IMF.

Matangazo ya kibiashara

Majaji wanaosikiliza kesi hiyo hapo jana wamesema kuwa kutokana na mazingira ya kesi yenyewe ilivyo na upande wa mashtaka kuonekana kutojipanga vizuri, wameamua kumuachia kiongozi huyo kutoka kifungo cha ndani ambapo sasa hata fedha za dhamana alizowekewa na mke wake zitarejeshwa.

Wakisoma maazimio ya mahakama, majaji hao wameongeza kuwa kuachiliwa huko toka kifungo cha ndani kwa Strauss-Kahn hakumaanishi kuwa mtuhumiwa huyo hana kesi ya kujibu kwani upelelezi utakapokamilika atakuwa hana budi kurejea mahakamani hapo kujibu mashtaka yanayomkabili.

Kabla ya kufanyika kwa kesi hiyo tayari wanasheria nchini Marekani walishabashiri kuwa kiongozi huyo ataachiliwa huru toka kifungo cha ndani hasa kutokana na kubainika kwa taarifa mpya kuwa mwanamke aliyemshtaki Strauss-Kahn alidanganya mara kadhaa katika ushahidi wake huku pia uraia wake kwa nchi ya Marekani ukibainika kuwa na kasoro kwa kudanganya.

Hata hivyo waendesha mashtaka wa mahakama hiyo wamesema kuwa licha ya mtuhumiwa huyo kuachiliwa toka kifungo cha ndani hawatafuta mashtaka ya kesi inayomkabili kiongozi huyo na kuwa wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na malalamiko ya mwanamke huyo muhudumu wa hoteli ambayo Strauss-Kahn alifikia wakati alipokuwa nchini humo.

Mawakili wanaomtetea mteja wao, wameonesha kufurahishwa na uamuzi huo wa mahakama na kuongeza kuwa huu ni udhibitisho tosha kabisa kuwa kesi dhidi ya mteja wao ni yakisiasa na kubambikizia na kuwa kiongozi huyo hana hatia dhidi ya mashtaka dhidi yake.

Wameongeza kuwa watahakikisha mteja wao anapata haki zake alizozipoteza ikiwa ni pamoja na kumfungulia mashtaka mwanamke huyo mwenye asili ya Guinea kwa kusema uongo na kuidanganya mahakama.