THAILAND-SHINAWATRA

Chama cha Yingluck Shinawatra chashinda uchaguzi nchini Thailand

Chama kikuu cha upinzani nchini Thailand kinachoongozwa na Yingluck Shinawatra kimeshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Yingluck Shinawatra mshindi wa kiti cha uwaziri mkuu wa Thailand
Yingluck Shinawatra mshindi wa kiti cha uwaziri mkuu wa Thailand REUTERS/Sukree Sukplang
Matangazo ya kibiashara

Chama hicho kimepata ushindi wa asilimia 92 ya kura zilizohesabiwa mpaka sasa na kufanikiwa kunyakua viti 260 kati ya viti 500 huku chama cha Demekrats kinachoongozwa na waziri mkuu absit Vejajiva kikiambulia viti 163.

Kufuatia ushindi huo waziri mkuu Vejajiva ametangaza kukubali matokeo na kukipongeza chama cha Puea thai kwa ushindi huo na kuahidi kushirikiana nacho katika kujenga demokrasia nchini humo.

Yingluck shinawatra ambaye ni dada wa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Thaksin Shinawatra anakuwa mwanamke wa kwanza kutoka ukanda wa asia ya kusini kuwa waziri mkuu.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wa chama chake Shinawatra amewashukuru wananchi hao kwa kukipa ushindi chama chake na kuahidi kufanya mabadiliko makubwa nchini humo.

Tayari Thaksin Shinawatra kaka wa Yingluck amempongeza dada yake kwa ushindi huo huku akitoa wito kwa chama kilichoshindwa kuonyesha ushirikiano kwa chama hicho.

Ushindi huo unamaliza mgogoro wa miaka mitano uliokuwa nchini humo ambapo mwaka jana wafuasi wa Thaksin Shinawatra wa Red Shirt walifanya maandamano makubwa kushinikiza kujiuzulu kwa serikali iliyoshindwa.