THAILAND

Zoezi la upigaji kura lamalizika nchini Thailand

Kiongozi wa Upinzani nchini Thailand Yingluck Shinawatra, anayepewa nafasi ya kushinda uchaguzi huo
Kiongozi wa Upinzani nchini Thailand Yingluck Shinawatra, anayepewa nafasi ya kushinda uchaguzi huo REUTERS/Stringer

Zoezi la upigaji kura nchini Thailand limemalizika ambapo kinachosubiriwa sasa ni kuanza kutangazwa kwa matokeo ya awali ya kura zilizokwishahesabiwa.

Matangazo ya kibiashara

Kufanyika kwa uchaguzi huo kunamaliza miaka mitano ya mgogoro wa kidemokrasia nchini humo baina ya kiongozi wa zamani wa nchi hiyo anayeishi uhamishono Thaksin Shinawatra na serikali.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanampa nafasi kubwa ya kuweza kushinda uchaguzi huo kiongozi wa upinzani toka chama cha Pheu Thai kinachoongozwa na dada wa aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Thaksin Shinawatra, Yingluck Shinawatra.

Yingluck anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo na kuweza kuwa mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo endapo atakishinda chama tawala kinachoongozwa na waziri mkuu Abhisit Vejjajiva.

Zaidi ya askari laki moja na elfu sabini wamesambazwa katika miji mbalimbali kulinda usalama kufuatia kuwepo kwa tishio la kuzuka kwa vurugu toka kwa wafuasi wa chama cha upinzani.

Mwaka jana nchi hiyo ilishuhudia maandamano makubwa zaidi kuwahi kufanywa nchini humo na wafuasi wa Red Shirt ambao wengi wanamuunga mkono waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra ambapo maelfu ya wananchi walijeruhiwa huku wengine wakiwa gerezani mpaka sasa.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa jioni ya hii leo.