Mazungumzo ya kitaifa yazinduliwa nchini Syria
Imechapishwa:
Syria imefungua mkutano wa mazungumzo ya kitaifa hapo jana, mazungumzo yanayoelezwa kufungua milango ya kuwepo kwa demokrasia ya vyama vingi baada ya chama tawala cha BAATH kutawala nchini humo kwa miongo mitano.
Takriban wawakilishi 200 walikuwa katika mazungumzo hayo wakiwemo wabunge wa kujitegemea na wanachama wa chama cha BAATH.
Akifungua mkutano huo,waziri mkuu wa Syria,Faruq al Sharaa amesema serikali yake itatangaza mabadiliko nchini humo kuelekea kwenye serikali ya demokrasia ya vyama vingi,itakayompa kila raia haki sawa katika kulijenga taifa hilo.
Sharaa amesema kwa muda wa wiki moja wizara ya mambo ya ndani itatekeleza uamuzi wa serikali wa kuondoa vikwazo kwa raia kurudi nchini Syria na kusafiri nje ya nchi hiyo.
Lakini wapinzani waligomea mkutano huo wakipinga vitendo vya unyanyasaji dhidi ya waandamanaji wanaopinga utawala wa rais wa nchi hiyo Bashar Al Assad.