OSLO-NORWAY

Mashambulizi yatikisa nchi ya Norway idadi ya vifo vya watu yazidi kuongezeka

Vifo zaidi vimeendelea kuripotiwa nchini Norway kufuatia mashambulizi mawili tofauti yaliyofanywa nchini humo, moja la mjini Oslo na jingine katika visiwa vya Utoeya baada ya mtu mmoja mwenye silaha kuwashambulia kwa risasi vijana waliokuwa wameweka kambi katika visiwa hivyo na kuua watu 84.

Online
Matangazo ya kibiashara

Shambulio lililofanywa kwenye visiwa vya Utoeya lilitokea muda mchache baadae baada ya kufanywa shambulio la bomu mjini Oslo kwenye ofisi za waziri mkuu wa nchi hiyo pamoja na wizara ya mafuta nchini humo ambapo watu saba walipoteza maisha na wengine wengi walijeruhiwa.

Akizungumzia shambulio la mjini Oslo waziri mkuu Jens Stoltenberg amesema kuwa miongoni mwa waliokufa ni pamoja na maofisa katika wizara yake ambapo hakuweza kuweka wazi majina ya watu ambao wamepoteza maisha katika shambulio hilo la bomu.

Muda mchache baadae wakati polisi wakiwa katika harakati za kuwaokoa watu walionusurika katika shambulio la bomu la mjini Oslo, wakapokea taarifa kuhusu uwepo wa mtu mmoja mwenye silaha katika visiwa vya Utoeya ambaye ameanza kuwashambulia watu walioweka kambi katika visiwa hivyo .

Polisi wanamshikilia raia mmoja wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 32 kuhusiana na mashambulizi ya siku ya ijumaa ambapo alikamatwa sentimita chache toka eneo ambalo alikuwa amesimama akiwashambulia vijana waliokuwa kwenye kambi hiyo jirani na mji wa Oslo.

Wakati huohuo vikosi vya polisi na vile vya jeshi la Norway vimeanza msako wa kuwatafuta watu zaidi waliohusika na shambulio hilo, ambapo ulinzi umeimarishwa katika majengo ya ofisi za serikali na maeneo ya watalii huku tahadhari ikitolewa kwa wananchi kuwa makini na maeneo wanayotembelea.

Katika taarifa zinazoendelea kupatikana toka nchini humo zinasema kuwa zaidi ya watu 90 wanasemekana kuuawa katika mashambulizi hayo ambayo mpaka sasa hakuna kundi ambalo limetaja kuhusika na mashambulizi hayo.

Polisi wanasema kuwa wamepokea taarifa ambazo wanazifanyia uchunguzi kuhusiana na mashambulizi hayo ambapo wanadai kuwa watu waliotekeleza shambulio hilo wanalenga kupinga kile ambacho serikali ya nchi hiyo imekifanya kwa kupeleka majeshi yake nchini Afghanistan na Libya.