SPAIN-ITALIA

Papa Benedict XVI awasili nchini Uhispania licha ya uwepo wa maandamano ya kupinga ziara yake

Papa Benedict XVI akibusu bilauli iliyowekwa damu ya Marehemu Papa John Paul II
Papa Benedict XVI akibusu bilauli iliyowekwa damu ya Marehemu Papa John Paul II REUTERS/Stefano Rellandini

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Benedict XVI amewasili nchini Uhispani katika Jiji la Madrid kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Siku ya Vijana Duniani ambazo zimeambatana na maandamano na ghasia nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Papa Benedict XVI amewasili nchini Uhispania akitokea Rome, Italia ambapo ameligusia suala la Uchumi na kuweka bayana ni lazima uchumi ushughulikia na maendeleo na mahitaji ya wananchi na siyo kwa ajili ya kupata faida pekee.

Ziara hii ya siku nne ya Kiongozi huyo wa juu Duniani wa Kanisa Katoliki inakuja wakati ambapo kumekuwa na upingaji mkubwa wa yeye kuzuru katika taifa hilo wakati huu ambapo hali ya uchumi imekuwa kitendawili.

Jeshi la Polisi limelazimika kukabiliana na vijana ambao wamejitokeza kupinga ziara ya Papa Benedict XVI na kuwalazimisha polisi kutumia risasi za mpira na mabomu ya machozi kuwatawanya.

Mahujaji wanaokadiriwa kufikia milioni moja kutoka duniani kote wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo za Siku ya Vijana Duniani zitakazodumu kwa siku sita ambapo Papa Benedict anatarajiwa kuhutubia.

Suala kubwa ambalo limekuwa likitikisa mataifa ya Ulaya ni kutetereka kwa uchumi ambapo Papa Benedict XVI ameweka bayana umefika wakati ambapo wananchi inabidi wafaidike na uchumi wa nchi zao.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki mwenye umri wa miaka themanini na nne kwa sasa amesema tatizo la kiuchumi lililopo kwenye maeneo mengi ni masuala ya ndani zaidi na si ya nje kama ambavyo yanashughulikiwa kwa sasa.

Kilio kikubwa nchini Uhispania kimeendelea kuwa ukosefu wa ajira ambapo ambao umefikia asilimia ishirini kitu ambacho kimemsukuma Papa Benedict XVI kusema juhudi zinatakuwa kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.