IRAQ-MAREKANI

Wanajeshi wa Marekani wanaoshika doria nchini Iraq kwa mara ya kwanza waepuka vifo

Wanajeshi wa Marekani kwa mara ya kwanza mwezi uliopita wameshuhudia hakuna kifo cha mwanajeshi yoyote katika kikosi chao kinacholinda doria nchini Iraq tangu wamefanya uvamizi na kuuangusha Utawala wa Marehemu Sadam Hussein mwaka 2003.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Majeshi ya Marekani Meja Angela Funaro amethibitisha kwa mara kwanza kutokuwepo kwa mauaji ya mwanajeshi wa nchi hiyo tangu kuanza kazi ya kushika doria nchini Iraq.

Kauli ya Marekani inakuja baada ya serikali ya Iraq kutoa takwimu za vifo katika mwezi wa Agosti ambazo zinaonesha watu mia mbili na thelathini na tisa kupoteza maisha ikiwa ni watu ishirini pungufu ukilinganisha na ilivyokuwa mwezi Julai.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara za Afya, mambo ya Ndani na Ulinzi zimeonesha kati ya watu hao wapo raia mia moja hamsini na watano, polisi arobaini na watano pamoja na wanajeshi thelathini na tisa.

Msemaji wa Majeshi ya Marekani Meja Funaro ameweka bayana wanajeshi wake kwa mara ya kwanza hawajakabiliwa na kifo hata kwa ugonjwa wala kwa ajali kitu ambacho hakikuwahi kutokea hapo awali.

Upungufu huu wa vifo vya wananchi wa Iraq na hata wanajeshi wa Marekani nchini humo unakuja kukiwa kumesalia miezi kadhaa kabla ya Majeshi ya nchi hiyo hayajakamilisha kazi yake ya kulinda doria iliyoanzaa mwaka 2003.

Katika hatua nyingine wafungwa kumi na nne ambao walikuwa wanakabiliwa na makosa ya Ugaidi nchini Iraq wamekimbia kwenye gereza walilokuwa wanashikiliwa baada ya kuchimba andaki.

Wafungwa hao wametoroka kwenye gereza la Al-Faisaliyah lililopo katika Jiji la Mosul na tayari Kanali Mohammed Al-Juburi amethibitisha kutoroka kwa wanajeshi hao waliochimba shimo la chini kwa chini.

Tayari msako mkali umeanza wa kuwasaka wale wote ambao wametoroka na hata waliofanikisha kutekelezwa kwa mpango huo na hatimaye watu hao kutorokea kusikojulikana.